Nuru FM

Mwanakijiji asalimisha silaha aina ya Gobole kwa Mhifadhi wa Ruaha

29 March 2023, 8:05 pm

Mkuu wa hifadhi ya Ruaha Godwel Ole Meing’ataki akipokea Silaha aina ya Gobole.

Elimu ya Uhifadhi inayotolewa na wahifadhi katika maeneo yanayozunguka hifadhi ya taifa ya Ruaha imesaidia wananchi kusalimisha silaha wanazotumia kufanya ujangili.

Na Vitor Meena

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Mkoani Iringa, imeendelea na ziara ya kuzungukia Vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo na kutoa elimu ya uhifadhi ikiwemo kupambana na ujangili ambapo mapema leo Mkazi wa Kijiji cha Matalawe Kata ya Mlowa Jimbo la Isimani amekabidhi silaha yake aina ya Gobole kwa Mkuu wa hifadhi hiyo ya Ruaha, Kamanda Godwel Ole Meing’ataki.

Mkazi huyo amesema, ameamua kusalimisha silaha hiyo aliyokuwa anaitumia Kwa ujangili wa kuwindia wanyama wa porini baada ya kupata elimu ya ujirani mwema ambapo zoezi la wananchi mbalimbali kusalimisha silaha zao kwa uwazi au kificho limeongezeka baada ya elimu inayoendelea kutolewa na Mkuu huyo wa hifadhi hada kwenye vijiji vinavyoizunguka hifadhi ya taifa Ruaha.

Meing’ataki ameongeza kuwa, ameamua kusimamia zoezi la kutoa elimu ya uhifadhi Kwa wananchi baada ya kuona hali ya ujangili inaongezeka ambapo hadi sasa vijiji vilivyo tembelewa na kupewa elimu ya uhifadhi ni pamoja na Kijiji Cha Kisilwa, Mahuninga, Makifu, Mapogoro, Idodi, Matalawe pamoja na kijiji Cha Tungamalenga ambacho ndicho kinachoongoza Kwa ujangili Kwa mujibu wa tafiti.

Hata hivyo, Meing’ataki amesisitiza kuwa ni jukumu la Kila mwananchi kujua umuhimu wa kulinda na kuhifadhi urithi tuliopewa na Mungu Ili tuweke kuwarithisha watoto na wajukuu wetu kama ilivyo kauli mbiu ya uhifadhi isemayo “Tumerithishwa, tuwarithishe.”