Nuru FM

TASAF wapewa wiki mbili kuwalipa wanufaika wa mpango huo

23 February 2024, 10:27 am

Waziri Simbachawene Akitoa maelekezo kwa Viongozi wa TASAF. Picha na Mwandishi wetu.

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameupa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) hadi Machi 5, mwaka huu uwe umelipa malimbikizo yote yanayodaiwa na walengwa wa mpango huo nchini kote.

“Uongozi wa pamoja umesaidia sana utekelezaji mzuri wa miradi hii ya TASAF. Lakini kuna kelele kubwa katika mradi huu, kelele hiyo ni ile inayohusu ucheleweshaji wamalipo kwa walengwa; Nasema tusimgombanishe Mheshimiwa Rais na walengwa. Ni haki yao kulipwa fedha zao kwa wakati na hiyo ndiyo njia itakayoondoa kelele hizo,” alisema.

Simbachawene ameyasema hayo katika ziara yake ya kutembelea wanufaika wa mradi huo unaolenga kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya watu waishio katika mazingira magumu aliyoifanya Iringa Vijijini katika vijiji vya Migori na Kinywang’anga jimboni Isimani.

Wakati katika kijiji cha Kinywang’anga kuna kaya 34 zilizotambuliwa na kuingizwa katika mpango huo unaohusu uhawilishaji (ugawaji) fedha kwa walengwa, ajira za muda na uwekaji akiba kupitia vikundi, katika kijiji cha Migori kuna kaya 117 zinazonufaika.

“Kwa kuwa kila kitu kipo sawa, lazima tuwasimamie mtoe malipo hayo kwa wakati. Mkifanya hivyo zaidi ya muda huu ambao tumekubaliana, serikali haiwezi kukubali na hatuwezi kumuacha mtu salama,” alisema bila kutaja kiwango kinachodaiwa.

Simbachawene alisema mpango wa TASAF ni wa kupigiwa mfano kwa kuwa unalenga kuongeza kipato cha kaya na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto, kuinua uchumi kwa kujenga uwezo kwa kaya katika utunzaji rasilimali na kutengeneza njia mbadala na endelevu za ajira na kushiriki katika kazi za jamii na kupata kipato cha ziada kwa matumizi ya chakula na kugharamia mahitaji mengine ya msingi huku wakiboresha miundombinu katika jamii na kupata ujuzi na stadi za maisha.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Venance Ntiyalundura alisema tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umewezesha mkoa wa Iringa wenye zaidi ya walengwa 30,000 kupata zaidi ya Sh bilioni 16.8 ambazo kati yake zaidi ya Sh bilioni 13 zimegaiwa kama ruzuku kwa wanufaika hao huku zinazobaki zikienda kwenye miradi inayotoa ajira za muda na kwa ajili ya vikundi vya kukopa na kurejesha.