PJT-MMMAM yataka baba kushiriki katika malezi ya Mtoto
25 July 2026, 16:45

Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuhakikisha baba anapata nafasi stahiki katika malezi ya watoto.
Na Adelphina Kutika
Wataalamu wanaotekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) katika halmashauri zote tano za Mkoa wa Iringa wametakiwa kuongeza ushiriki wa kina baba katika malezi na makuzi ya watoto ili kujenga kizazi bora kitakachofikia matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Akifungua kikao cha robo ya tatu cha utekelezaji wa programu hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Asheri Mdalila, amewataka wataalamu kuhakikisha elimu inayotolewa kwa jamii inawafikia na kuwahusisha kwa karibu kina baba, akisisitiza kuwa malezi si jukumu la mama pekee bali ni wajibu wa wazazi wote.
Amesema ushiriki wa baba katika malezi ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata ulinzi, upendo, lishe bora na mazingira salama ya kukua na hivyo kuwa na maendeleo mazuri ya kimwili, kiakili na kijamii.
Kwa upande wake, Mratibu wa PJT-MMMAM Mkoa wa Iringa, Martine Chuwa, amesema kikao hicho kimetoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika robo ya tatu ya utekelezaji wa programu, kubaini changamoto zilizojitokeza pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wake.
Amesema miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuhakikisha baba anapata nafasi stahiki katika malezi ya watoto huku jamii ikiendelea kuondokana na mitazamo na tamaduni zinazoweza kuzuia ushiriki wa wanaume katika jukumu hilo.
Naye Mratibu wa Mradi wa Mtoto Kwanza kutoka Shirika la IDYDC, John Nkoma, amesema wataalamu wanapotoa elimu kwa jamii wanapaswa kuzingatia masuala ya jinsia, hususan kuongeza ushiriki wa baba katika malezi, kwa kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano wa wazazi wote.
Ameongeza kuwa ni muhimu pia kuzingatia suala la ujumuishi kwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa programu hiyo ili kunufaika na huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Baadhi ya wataalamu walioshiriki kikao hicho wamesema maazimio yaliyofikiwa yataongeza ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za malezi na makuzi ya awali ya mtoto, hasa katika maeneo ya lishe, na malezi katika familia.