Forland yazindua kampeni ya kuzuia na kudhibiti moto Kilolo
19 September 2026, 07:54

Kampeni hiyo inalenga kuimarisha ulinzi wa misitu, mazingira pamoja na vyanzo vya maisha ya wananchi.
Na Hafidh Ally
Shirika la FORLAND kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, limezindua Kampeni ya Kuzuia na Kudhibiti Moto katika Kata ya Bomalang’ombe, Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa.
Uzinduzi huo uliofanyika katika Kijiji cha Wangama umebeba kaulimbiu “Misitu Yetu Uchumi Wetu: Usichome Moto Ovyo”, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu madhara ya moto usiodhibitiwa na umuhimu wa kuchukua hatua za mapema katika kuzuia na kudhibiti majanga ya moto katika maeneo ya misitu na ardhi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, jamii, wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali katika kulinda misitu na mazingira dhidi ya moto.
Amesema hatua hizo zinapaswa kuhusisha uzuiaji wa moto, ufuatiliaji, utayari pamoja na udhibiti wa moto kwa wakati, sambamba na kuimarisha ushiriki wa jamii katika usimamizi endelevu wa misitu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa FORLAND Mkoa wa Iringa, Nyachia Robert, amesema shirika hilo limeendelea kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya majanga ya moto kupitia kamati za vijiji, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.

Naye mwakilishi wa Muhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilolo, Yakob Lukumay, amesema taasisi hiyo ina utaratibu wa kugawa miche ya miti bure kwa wananchi kwa lengo la kuendeleza uhifadhi wa mazingira.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya majanga ya moto wilayani Kilolo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Bi. Siwema Jumaa, amesema zaidi ya hekta 1,000 zimeteketea kwa moto.
Amesema miongoni mwa sababu zilizobainika ni uchomaji wa mkaa pamoja na matumizi ya moto wakati wa uandaaji wa mashamba.
Kupitia kampeni hiyo, FORLAND na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa zinaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda misitu, wakisisitiza kuwa uhifadhi wa misitu ni kulinda uchumi, mazingira na maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ujumbe mkuu wa kampeni ukiwa:“MISITU YETU UCHUMI WETU: USICHOME MOTO OVYO.”
