Nuru FM
Nuru FM
6 June 2025, 12:09

Hatua hiyo imejiri baada ya takwimu kuonesha kuwa mkoa wa Iringa ulikuwa na changamoto ya Udumavu kwa 56.9 kwa mwaka 2022 jambo lililopekekea kutekeleza afua mbalimbali za lishe katika jamii.
Na Hafidh Ally
Katika kukabiliana na changamoto ya Udumavu Mkoani Iringa, Serikali kwa kushirikiana na asasi za Kiraia imefanikisha upatikanaji wa chakula kwa watoto shuleni kwa asilimia 90.
Akizungumza katika kikao cha Tathmini ya Lishe cha Robo ya Tatu January- March 2025, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dr. Silvia Mamkwe amesema kuwa serikali imeendelea kuimarisha hali ya lishe kwa kuhakikisha vyakula vinavyopikwa shuleni vina virutubisho vinavyohitajika.
“Kwa sasa upatikanaji wa chakula shuleni ni zaidi ya asilimia 90 na katika shule tunahamasisha walime mbogamboga, matunda na kufundishwa namna ya kuandaa chakula bora” Alisema Dr. Mamkwe
Akizungumzia hali ya lishe kwa mwaka 2025, Dr. Silvia amebainisha kuwa walishikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania TFNC na kufanya utafiti mdogo na kubaini kwa sasa Udumavu umepungua kutoka asilimia 56.9 Mpaka asilimia 31 kwa mkoa wa iringa.
“tunaamini katika utafiti ujao wa mwaka 2027 Mkoa wa iringa utakuwa vizuri kwa sababu kwenye malezi na makuzi ya watoto hali imeendelea kuwa vizuri.

Kwa upande wake Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Iringa Mwl. Reginaldo Msendekwa anayeratibu masuala ya Lishe Shuleni, kwa sasa katika mkoa wa Iringa umefanikiwa kuhamasisha wazazi kuwapatia chakula shuleni kwa asilimia 90 kupitia waraka wa elimu No. 3 wa mwaka 2016.
“katika Mkoa wa Iringa tumefanikiwa katika utoaji wa chakula kwa shule za msingi kwani, Manispaa ya Iringa wanatoa chakula kwa asilimia 82.7, Iringa Vijijini kwa asilimia 97.2, Mufindi asilimia 97.8, Mafinga asilimia 77.5 na Kilolo kwa asilimia 93.3” Alisema Mwl Msendekwa
Akizungumzia dhana ya wananchi kutumia vyakula vilivyoongezwa virutubisho, Mwenyekiti wa chama cha wasindikaji Mkoa wa Iringa Benedict Myema amesema kuwa kwa sasa wananchi wamekuwa na mapokeo mazuri baada ya kutoa elimu kwa wananchi ambao walidhani kutumia bidhaa hizo kutawaletea madhara.
“wataalamu wa lishe wamekuwa wakishirikiana na sisi kuwahamasisha wananchi kutumia bidhaa za kusindika zenye virutubisho, kama unga ulioongezwa virutubisho, maharage lishe na sasa imesaidia wananchi kuwa na afya njema, hasa wanawake kuzaa watoto wasiokuwa na magonjwa kama vichwa vikubwa, Migongo wazi na wenye midomo ya sungura” Alisema Myema
Kikao hicho kimehudhuriwa na maafisa Lishe, wataalamu kutoka Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, na Taasis Binafsi wakiwemo TAHEA na Harvest Plus.
