Nuru FM

TFS Mufindi yawanoa vijana kukabiliana na moto

24 June 2026, 09:49

Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Sao Hill, PCO Said Singano Akizungumza na wasailiwa. Picha Na Hafidh Ally

Mafunzo hayo yatasaidia kupata vikosi maalumu vya kuzuia, kudhibiti na kuzima moto katika maeneo ya shamba na maeneo yanayolizunguka.

Na Hafidh Ally

Zaidi ya vijana 200 kutoka vijiji 61 vinavyozunguka Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill, Wilaya ya Mufindi, wamepata mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhifadhi wa misitu na mazingira.

Akizungumza wakati wa usaili wa vijana zaidi ya 400 waliojitokeza kupima utimamu wa mwili na akili, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Sao Hill, PCO Said Singano, amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za kuhakikisha wananchi wanaozunguka shamba hilo wanashiriki kikamilifu katika kulinda misitu dhidi ya majanga ya moto.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo vijana katika mbinu za kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na moto wa misitu, pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kulinda rasilimali za taifa.

Alisema idadi ya waombaji imekuwa kubwa kuliko nafasi zilizotangazwa, jambo linaloonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa misitu. Hata hivyo, alibainisha kuwa shamba lina shughuli nyingine zinazohitaji nguvu kazi, ikiwemo usafi wa mashamba na kazi za bustani, hivyo baadhi ya waombaji ambao hawatapangwa kwenye vikosi vya moto wanaweza kushirikishwa katika majukumu hayo.

Kwa upande wake, Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mufindi, Sajenti Guntramu Mlenge, amesema ushirikiano kati ya jeshi hilo na Sao Hill umeendelea kuzaa matunda kupitia utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto.

Kwa upande wao baadhi ya vijana waliojitokeza kupata mafunzo hayo wamesema kuwa hatua hiyo itasaidia kukabiliana na majanga ya moto kwani misitu imekuwa na faidha katika maisha ya binaadamu.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti Sao Hill imekuwa na utaratibu wa kukabiliana na majanga ya moto wa misitu kwa kuendesha usaili wa watumishi wa muda watakaounda vikosi maalumu vya kuzuia, kudhibiti na kuzima moto katika maeneo ya shamba na maeneo yanayolizunguka.