Nuru FM

RC kheri ahimiza ukusanyaji mapato Iringa

15 April 2026, 09:21

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akizungumza kwenye kikao cha tathimini ya utendaji kazi kwa viongozi. Picha Ayoub Sanga

“Haiwezekani viongozi hao kujikita katika matumizi ya fedha pekee bila kuwa na mikakati madhubuti ya ukusanyaji wa mapato”

Na Ayoub Sanga

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewaagiza wenyeviti wa halmashauri za wilaya  kufanya tathmini ya kina ya hali ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, na  kuongeza ubunifu, uwajibikaji ili kuchochea ongezeko la mapato hayo.

Mh. Kheri ameyasema hayo wakati akiongoza kikao maalumu cha tathimini ya utendaji kazi kwa viongozi mbalimbali ngazi ya Halmashauri na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kupunguza utegemezi wa Serikali Kuu.

Sauti ya RC Kheri

Mhe. Kheri amesisitiza kuwa baadhi ya halmashauri zimeonyesha kufanya vizuri katika eneo hilo, lakini bado kuna haja kwa nyingine kujifunza na kuiga mifano bora ili kuongeza ufanisi wa jumla wa ukusanyaji wa mapato katika mkoa huo.

Naye Katibu Tawala Msaidizi (Sehemu ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi) Rehena Ntahena amesema hadi kufika mwezi Machi Halmashauri mkoani Iringa zilikusanya Shilingi Bilioni 29.6 (67%) ya makisio ya kukusanya Bilioni 44.1 kwa mwaka.

Sauti ya Rehena

Kwa upande wao wenyeviti Halmashauri za Wilaya Mkoani Iringa wameahidi kwenda kufanya tathmini ya ukusanyaji mapato kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi za wakurugenzi wa Halmashauri ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Sauti ya Wenyeviti Halmashauri

Viongozi hao wanajukumu la kusimamia kwa karibu vyanzo vyote vya mapato, kubaini mianya ya upotevu na kuweka mikakati madhubuti ya kuibua vyanzo vipya vinavyoendana na mazingira ya maeneo yao sambamba na usimamizi thabiti wa fedha za umma ili kuleta maendeleo endelevu.