Ngajilo awawezesha wajasiriamali 400 Iringa
2 June 2026, 11:23

Mafunzo hayo, ambayo ni msimu wa pili kufanyika, yamelenga kuwapa wajasiriamali wadogo na wa kati maarifa ya kisasa kuhusu usimamizi wa biashara, upatikanaji wa mitaji, masoko na fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuongeza tija na mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Na Hafidh Ally
Zaidi ya wajasiriamali 400 kutoka Manispaa ya Iringa wameshiriki mafunzo maalumu ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini yakilenga kuwajengea uwezo wa kusimamia na kukuza biashara zao kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewahimiza wajasiriamali kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo mikopo kupitia Halmashauri pamoja na kujisajili katika mifumo ya manunuzi ya umma ili waweze kushiriki kikamilifu katika zabuni na kuongeza mapato ya biashara zao.
Alisema katika mazingira ya sasa ambapo idadi ya wahitimu inaongezeka kila mwaka, ujasiriamali unapaswa kupewa kipaumbele kama suluhisho la changamoto ya ajira na njia ya kuongeza kipato kwa wananchi.
“Tunapowajengea uwezo wananchi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, tunawapa nyenzo za kujikwamua kiuchumi, kuanzisha ajira kwa wengine na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla,” alisema Sitta.

Kwa upande wake, Katibu Msaidizi kutoka Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Hassan Rafiq, amesema mwitikio wa washiriki katika msimu huu wa pili umekuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na mafunzo ya awali, jambo linaloonesha hamasa ya wananchi kutafuta maarifa yatakayowawezesha kukuza biashara zao.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea washiriki uwezo katika maeneo ya usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, upatikanaji wa masoko, matumizi ya teknolojia na namna ya kunufaika na mifumo rasmi ya kifedha kutoka Serikali na taasisi za fedha.
“Mheshimiwa Ngajilo anaamini maendeleo ya kweli yanaanza pale wananchi wanapopata maarifa ya kujitegemea kiuchumi. Ndiyo maana ameendelea kusukuma programu hizi za mafunzo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Rafiq.
Kwa upande wao Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na maudhui yaliyowasilishwa wakisema yamewapa uelewa mpya kuhusu namna ya kuendesha biashara kwa faida, kutafuta masoko na kutumia fursa za mikopo zinazopatikana kupitia taasisi mbalimbali.
Kupitia mafunzo kama hayo, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kuingia katika uchumi rasmi, kuongeza kipato cha kaya na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuijenga Tanzania yenye uchumi imara na jumuishi.