Nuru FM
Nuru FM
21 April 2026, 08:36

“Serikali haitavumilia vitendo vinavyowaongezea gharama zisizo za lazima wazazi na walezi”
Na Ayoub Sanga
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameendelea kusisitiza kuchukuliwa hatua kali dhidi ya Wakuu wa shule wanaokiuka utaratibu wa Serikali kwa kuanzisha michango isiyoidhinishwa.
Akizungumza katika kikao maalum cha tathmini ya utendaji kazi kilichowakutanisha viongozi wa ngazi ya halmashauri, wakiwemo Wakurugenzi, Madiwani pamoja na wajumbe wa Kamati, Mkuu wa Mkoa huyo ameagiza kuvuliwa madaraka mara moja Wakuu wote wa shule watakaobainika kuhusika.
Amesema vitendo hivyo ni ukaidi wa wazi dhidi ya mamlaka, huku baadhi ya Wakuu wa shule wakijipa madaraka yasiyowahusu na kufanya maamuzi kinyume cha taratibu zilizowekwa.
Aidha Mh. Kheri amemuagia Katibu Tawala Mkoa wa Iringa kufuatilia wakuu wa shule wenye tabia za kuchangisha michango na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwasimamisha kazi.
Amesisitiza kuwa Serikali tayari imeweka utaratibu wazi kuhusu michango mashuleni, sambamba na maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, hivyo hakuna sababu ya ukiukwaji huo.
Ameongeza kuwa juhudi za Serikali ni kupunguza mzigo kwa wananchi, na haitavumilia vitendo vinavyowaongezea gharama zisizo za lazima wazazi na walezi.