Nuru FM

Wanaume wa mahanzi iringa wapigwa na wake zao

3 September 2021, 9:01 am

Iringa

Na Hafidh Ally

Wanaume wa Kijiji cha Mahanzi Kilichopo Kata ya Wasa Wilaya ya Iringa wamelalamikia vitendo vya wanaume kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kupigwa na wake wao.

Wakizungumza katika  Ziara ya kikazi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mh. Mohamed Hassan Moyo iliyopewa jina la ULIPO NIPO TOA KERO YAKO TUIPATIE MAJAWABU SEMA UKWELI NA SIYO MAJUNGU baadhi ya wanaume wa kijiji hicho wamesema kuwa wamekuwa wakipigwa na wake zao jambo ambalo linawaathiri kisaikolojia.

Wanaume hao wamesema kuwa wamekuwa wakipigwa na wake zao na mwenyekiti wa kijiji anazo taarifa za wao kupigwa.

“Kwa kweli sisi wanaume tunapigwa sana, yaani tunafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na tunashindwa kutoa Taarifa kutokana na mila zetu sisi wahehe” wamesema wanaume wa Mahanzi.

Aidha wanaume hao wameiomba serikali kuingilia kati kuhusu vitendo hivyo kwani vimekithiri katika kijiji chao.

Akijibia changamoto ya Wanaume kupigwa kwa Niaba ya OCD Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Iringa, Afande A.A MALEMA ambaye ni mkuu wa Kituo cha Polisi Ifunda amesema kuwa jeshi la polisi limeanzisha kitengo cha dawati la jinsia ambalo linahusika na matukio hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Moyo amesema kuwa ni kosa la Jinai kumpiga mtu hata kama amefanya kosa huku akiwataka wananchi wa kijiji hicho kwenda kuripoti matukio hayo ya ukatili wa kijinsia.