Nuru FM

4 July 2022, 3:57 pm

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara Mhe. Anne Makinda ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekutana na kuzungumza na wadau mkoa wa Shinyanga leo Jumatatu Julai 4,2022 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Shinyanga yenye lengo la kutoa elimu ya Sensa na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23,2022.


Makinda amesisiza Uzalendo kwa wananchi ili kufanikisha zoezi hili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa huku akiomba Hamasa ya Sensa ya watu na makazi iendelee hadi siku ya Sensa Agosti 23,2022.

“Siku ya sensa wananchi wanatakiwa kutoa taarifa za ukweli. Msiwafiche watu wenye ulemavu”,amesema Makinda.

“Taarifa za watu wenye ulemavu zikusanywe ili kusaidia serikali kupanga mipango kwa watau wenye ulemavu ili wapate huduma wanazotakiwa wapate”,ameongeza

Wale wapangaji wako katika nyumba ni kaya, wewe mwenye nyumba siyo kaya. Wapangaji kwenye nyumba yako watahesabiwa kuwa ni kaya. Kila mtu aliyelala ndani ya mipaka ya Tanzania watahesabiwa. Sensa itafanyika Tarehe 23 hadi 28 Agosti, Mkuu wa kaya awe na taarifa za watu waliolala usiku wa Agosti 23,2022″,amesema Makinda.

Naye Mtakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Pastory Ulimali amesema Dodoso la Sensa litakusanya taarifa za kaya siyo familia huku akibainisha kuwa  siyo lazima mkuu wa kaya awe baba au mama, wanaweza kutoa maelekezo kwa mtu mwingine katika kaya kwa niaba ya mkuu wa kaya.

“Sensa hii inawahusu watu wote awe mgeni mwenyeji, ili mradi huyo mtu amelala ndani ya mipaka ya Tanzania usiku wa Agosti 23,2022. Kila ahesabiwe mara moja tu na kila mmoja afanye uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi. Na kwa mara ya kwanza nchini Tanzania tutahesabu pia majengo”,amesema Ulimali.