Nuru FM

Rais Samia afanya mabadiliko madogo Baraza la Mawaziri

6 July 2023, 10:31 am

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan

Na Mwandishi wetu

RAIS Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kuunda wizara mpya.

Rais Samia amevunja Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na kuunda Wizara tatu; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Katika Mabadiliko hayo, amemteua aliyekuwa Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji.

Pia amemteua aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Fedha. Uteuzi huo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji ofisi ya Rais.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Mjini Lilongwe leo Julai 5, 2023 imesema Rais amemteua aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. 

Katika hatua nyingine Rais Samia amemteua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango akishughulikia Usimamizi wa Uchumi, Lawrence Nyasebwa Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa. 

Na amemteua aliyekuwa Kamishna Idara ya Uchambuzi wa Sera katika Wizara ya Fedha na Mipango, Elijah Mwandumbya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi wa Uchumi).