Nuru FM
Nuru FM
13 May 2026, 09:18

Msaada huo wa saruji unatarajiwa kuboresha uwanja wa mpira wa kikapu, huku kompyuta hizo zikilenga kuongeza ufanisi katika matumizi ya TEHAMA.
Na Hafidh Ally
Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mh. Jackson Kiswaga amekabidhi mifuko 200 ya saruji pamoja na kompyuta 42 kwa Uongozi wa Shule ya Tosamaganga ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na shughuli za michezo shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano Shuleni hapo Kiswaga amesema Msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi katika matumizi ya Tehama huku akiahidi kuendelea kushirikiana na shule hiyo kongwe kuimarisha mazingira bora ya elimu kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya Tosamagang Mwl. Lauren Manga amemshukuru Mbunge Kiswaga kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya shule hiyo, akieleza kuwa msaada huo utasaidia kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu na michezo.

Awali Diwani wa Kata ya Kalenga, Shakira Kiwanga amemshukuru Mh. Kiswaga kwa mchango wake wa kuwaunganisha wadau mbalimbali wa maendeleo na kusaidia kupatikana kwa mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa shuleni hapo.
Kwa upande wao wanafunzi wa shule hiyo wamesema kuwa uwepo wa Kompyuta hizo utasaidia wanafunzi kujifunza zaidi matumizi ya Tehama kwa wanafunzi wanaosomea masomo ya Kompyuta.