Nyalumbu Fc yawa mabingwa wa bonanza la Kitonga marathon 2026
29 October 2026, 11:18

Bonaza hilo limehusisha Vijiji 80 na Kata 20 za Wilaya ya Kilolo ikiwa ni maandalizi ya Kitonga Marathon 2026.
Na Hafidh Ally
Timu ya Nyalumbu FC imeibuka mabingwa wa jumla wa Bonanza la Kitonga Marathon 2026 baada ya kuifunga timu ya Kilolo kwa mabao 4-2, katika maandalizi ya mbio za Kitonga Marathon zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2026, wilayani Kilolo, mkoani Iringa.
Bonanza hilo limelenga kuhamasisha wananchi kushiriki mbio hizo, zinazotarajiwa kuimarisha utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa maliasili za Mlima Kitonga, kutangaza fursa za uwekezaji na kukuza utalii wa asili pamoja na utalii wa michezo.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Fredy Mwakibete, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo, akisema zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki, hatua inayoweza kuongeza shughuli za kiuchumi na kipato kwa wananchi.
Amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama imejipanga kuhakikisha usalama wa washiriki na wananchi unazingatiwa wakati wote wa mbio hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Siwema Jumaa, amesema mbio hizo zitahusisha kilomita 5, 10 na 21, pamoja na mbio za kupanda Mlima Kitonga.
Naye Mratibu wa Kitonga Marathon 2026, Lucy, amesema washindi watapata zawadi kulingana na hatua ya mashindano. Katika ngazi ya kata, mshindi wa kwanza atapata shilingi 50,000, huku mshindi wa kwanza ngazi ya tarafa akipata shilingi 100,000.
Ameongeza kuwa katika fainali ya wilaya, mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi 150,000, mpira mmoja na seti moja ya jezi, huku mshindi wa pili akipata shilingi 100,000, mpira mmoja na seti moja ya jezi.
Kitonga Marathon 2026 inatarajiwa kuwa jukwaa la kuhamasisha michezo, kutangaza vivutio vya Mlima Kitonga na kuchochea shughuli za kiuchumi kupitia utalii na fursa za uwekezaji wilayani Kilolo.