Nuru FM

Dkt Linda: “Madiwani hamasisheni wananchi kujiunga na bima ya afya”

13 November 2026, 08:14

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, akizungumza katika baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga. Picha na Hafidh Ally

Mpango wa Bima ya afya kwa wote unalenga wananchi kujilipia bima ya afya ili kujihakikishia uhakika wa matibabu kabla ya magonjwa hayajatokea.

Na Hafidh Ally

Madiwani wa Halmashauri ya Mji Mafinga wametakiwa kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwawezesha kupata huduma za matibabu kwa urahisi na kupunguza changamoto za gharama za matibabu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Luganga ambapo amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuunga mkono mpango huo na kuuelezea kwa usahihi ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma za matibabu.

Sauti ya DC Linda

Dkt. Salekwa amesema kuwa Bima ya Afya kwa Wote Awamu ya Pili ilizinduliwa rasmi mkoani Iringa Oktoba 22, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, hivyo ni muhimu kwa madiwani kushiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huo.

Sauti ya DC Linda

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mh. Reginant Kivinge amesema kuwa madiwani wamepokea agizo hilo la Mkuu wa Wilaya na wataanza kutoa elimu kwa wananchi kujua umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kwa wote.

Sauti ya Kivinge

Akizungumzia faida za kujiunga na Bima ya afya kwa wote, Mkuu wa Idara ya afya Halmashauri ya Mji Mafinga Dr. Boniventura Chitopela amesema Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote nchini Tanzania unagharimu Shilingi laki moja na nusu (TZS 150,000) kwa mwaka kwa ajili ya mwanachama na familia yake yenye jumla ya watu sita (6) kupata huduma za afya.

Sauti ya Boniventura

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele Villa, amewataka madiwani na wataalamu wa Halmashauri hiyo kuwa mabalozi wazuri wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo.