Nuru FM

Mbunge Nyamoga aanza ziara Kilolo, barabara yawa kero kubwa

25 April 2024, 9:50 am

Mbunge wa Jimbo la Kilolo Justine Nyamoga akishuhudia Jinsi miundombinu ya barabara ilivyo katika Jimbo lake. Picha na Clement Sanga.

Mvua zinazoendelea kunyesha hapa Nchini zimesababisha uharibifu katika Barabara hasa eneo la Katika jimbo la Kilolo Mkoani Iringa.

Na Mwandishi wetu

Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mkoani Iringa Justin Nyamoga amefanya ziara ya kutembelea barabara zilizopo katika Kijiji cha Lulindi kata ya Ukwega na Kijiji cha Mlafu wilayani humo ili kujionea hali halisi ya barabara hizo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mbunge Nyamoga amefanya ziara hiyo katika vijiji hivyo akiambatana na Wakala ya barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wakala ya barabara mjini na vijijini (TARURA) ili kuona namna wavyoweza kusaidia kutatua changamoto wanazokumbana nazo wananchi kutokana na uharibifu wa barabara hizo uliosababishwa na mvua.

Akiwa katika barabara ya Lulindi Mbunge Nyamoga akalazimika kusimamisha ziara na kushiriki zoezi la kusaidia kuliondoa gari la kubeba wagonjwa lililokwama katika barabara hiyo, ambalo limeshindwa kuendelea na kazi ya kubeba wangonjwa wa dharula wanaohitaji kusafirishwa kwenda katika hospitali ya Rufaa.

“Licha ya kuwa niliambiwa huku mvua kubwa inaendelea kunyesha nikaona siwezi kukaa nisubiri mvua iishe ili nije, nimekuja na wataalamu ili waangalie wanawasaidiaje hata kwa kuweka changarawe ili barabara ipitike kwa muda tukisubiri ukarabati mkubwa pindi mvua zitakapoisha”, amesema Nyamoga.

Mvua inayonyesha katika maeneo mbalimbali nchini imeendelea kuleta athari mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya madaraja na barabara huku Kilolo ikiwa ni mwiongoni mwa maeneo yalipata changamoto hiyo na kumlazimu Mbunge Nyamoga kuandaa ziara ya kutembelea barabara zote za Jimbo hilo,na anatarajia kumaliza Aprili 27, 2024.