Nuru FM

Halima Mdee na wenzake 18 wafukuzwa CHADEMA

12 May 2022, 7:07 am

Kamati Kuu ya CHADEMA imepiga kura na kuwafukuza wanachama 19 wanawake waliokuwa wanashutumiwa kwa utovu wa nidhamu kwa kosa la kuapishwa kuwa wabunge bila ruhusa ya chama chao.

Kikao hicho ambacho kimechukua muda mrefu baada ya mkutano wa Baraza Kuu uliofanyika Mlimani City Dar es Salaam, kimeisha kwa kura za Matokeo ya jumla ya Idadi ya wajumbe 423, Waliokubalina na maamuzi ya Kamati ya kuwafukuza Uanachama ni 413 sawa 97.6%, Wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati kuu ni 5 sawa na 1.2%, na wasiofungamana na upande wowote ni 5 sawa na 1.2%.

Wanawake wa Chadema Bawacha,waliofukuzwa ni makada waliokuwa mstari wa mbele kukipigania chama hicho na baada ya Bazara Kuu kubariki uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kuwafukuza ndani ya chama kwa kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge kinyume cha matakwa ya chama hicho.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema kwa sasa hakuna nafasi nyingine kwa waliokuwa makada 19 wa chama hicho ya kukata rufaa.

Pia, amesema hatua inayofuata ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuandika barua ya kumtaarifu Spika wa Bunge kuhusu uamuzi uliofanywa na baraza kuu kwa hatua zaidi ikiwemo ya kutangazwa kuvuliwa ubunge.

Aliyekuwa mwanachama wa Chadema, Halima Mdee amesema hakukuwa na uhuru kwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho katika upigaji wa kura na kwamba, kilichofanyika ni uhuni.

Nae Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe alipoulizwa baada ya kutoka hapo alisema hawakuwa na namna nyingine ya kufanya zaidi ya kufuata katiba.

Awali spika wa Bunge la Tanzania Tulia Ackson alisema kuwa hatma ya wabunge hao, itategemea matokeo michakato halali ya ndani ya chama. Kama mchakato wa usiku wa jana utaonekana halali, wabunge hao wanaweza kuvuliwa ubunge , kwa kuwa sheria ya Tanzania inaeleza iwapo mbunge atafukuzwa uanachama na chama kilichompeleka bungeni, ubunge wake utakoma.