Nuru FM

Mbolea ya ruzuku yamweka matatani mfanyabiashara Iringa

6 July 2023, 10:39 am

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Allan Bukumbi

Na Frank Leornad

SERIKALI ya Mkoa wa Iringa imemnasa mfanyabiashara Maneno Yusuph Kivembele (50) mkazi wa Ilula wilayani Kilolo akihususishwa na tuhuma ya ununuzi wa mbolea ya ruzuku kwa njia ya udanganyifu na kuuza kwa wakulima kwa bei ya juu kinyume na mpango wa serikali.

Taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego aliyesema serikali inaendelea kuwasaka watu wengine wanaojihusisha na hujuma hiyo.

Wakati akikamatwa hivi karibuni alisema mtuhumiwa huyo alikuwa amekwishanunua mifuko 627 ya aina mbalimbali ya mbolea kutoka kwa mawakala na makampuni  tofauti ya mbolea wilayani Iringa na Kilolo.

“Tumemkamata kwa makosa  kadhaa yakiwemo ya kuuza mbolea yenye ruzuku kwa wakulima kwa bei ya kati ya  Sh 82,000 na Sh 87,000 kwa  mfuko  mmoja wa  kilo 50 kinyume na taratibu,” alisema.

Makosa mengine ni pamoja na kuuza mbolea bila  leseni na kununua mbolea kwa kutumia vitambulisho vya wakulima  wengine kinyume na utaratibu  wa  serikali katika usambazaji wa mbolea yenye ruzuku.

“Baada ya kupata taarifa zake na kuwekewa mtego alinaswa na kufikishwa kituo cha polisi cha Lugalo wilayani Kilolo anakoendelea kushikiliwa hadi sasa,” alisema.

Akizungumzia jinsi mtuhumiwa huyo alivyofanya udanganyifu huo, Mkuu wa Mkoa alisema katika manunuzi yake mtuhumiwa alinunua mbolea  kutoka  kampuni ya ETG Inputs Limited kwa  kutumia namba ya mkulima 81140702890 ambayo  iliandikishwa  katika  mfumo wa ruzuku kwa jina la Sudiana J . Mwakalinga wa  wilaya ya  Mvomero mkoani Morogoro.

Baada ya kufuatilia usajili wa mkulima  kwenye mfumo ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo  alifanya  udanganyifu  wakati wa kujiandikisha na kujipatia namba tatu za ruzuku ambazo  ni 84050311708 kwa  ajili ya ekari saba, namba 84050327582 kwa ajili ya ekari 80 na namba 84050328057 kwa  ajili ya ekari 120 zote zikiwa ni za kijiji cha Ilula sokoni wilayani Kilolo .

“Taarifa  zote hizo zilikuwa za uongo  na kinyume na  utaratibu  unaotaka mkulima  kujisajili mara  moja kwenye kijiji  husika,” alisema.

Kwa  upande  wake  Michael  Sanga  ambaye  ni  Meneja  wa Kanda wa  Mamlaka  ya Mbolea  Tanzania Kanda ya  Nyanda  za  Juu  kusini alisema mtuhumiwa amekamatwa ikiwa ni  matokeo ya ofisi yake na ofisi ya  mkuu wa  mkoa katika  kudhibiti udanganyifu  katika mbolea hiyo ya ruzuku.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kwamba wanaendelea uchunguzi  zaidi wa suala hilo linalohisiwa kuhusisha mtu zaidi ya mmoja kabla ya mtuhumiwa huyo hajafikishwa mahakamani.