Heche awasili Iringa kuhutibia wananchi kesho
12 June 2026, 17:36

Na Hafidh Ally
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA bara , John Heche amewasili Mkoani Iringa leo 12 Juni 2026 Kwa ajili ya kufanya ziara na kuhutubia wanachama na wakazi wa Iringa.
Heche amewasili na kupokelewa na wanachama wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini ambapo Leo atazindua matawi mawili ya Chadema katika Eneo la Semtema na Mafifi huku akitarajiwa kufanya Mkutano wa hadhara kesho kuanzia saa 6 mchana katika Uwanja wa Mwembetogwa.
Mara baada ya kuwasili, Heche alipokelewa na viongozi na wanachama wa chama hicho wa Jimbo la Iringa Mjini, ambapo alishiriki shughuli mbalimbali za chama ikiwemo uzinduzi wa matawi mapya katika maeneo ya Semtema na Mafifi.

Akiwa mkoani Iringa, Heche anatarajiwa kufanya mkutano wa hadhara kesho Juni 13, 2026 kuanzia saa 6 mchana katika Uwanja wa Mwembetogwa.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wanachama wa CHADEMA pamoja na wakazi wa Iringa, ambapo atapata fursa ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na maendeleo yanayohusu wananchi.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa na wanachama wa Chadema, Heche kuwa licha ya Chadema kupitia changamoto katika kutekeleza majukumu yao ya kisiasa, watasimama imara kwa ajili ya kuwasemea wananchi.
“Chama chetu tumepitia misukosuko mara baada ya kuchaguliwa na hii ni kwa sababu tunasimamia haki, na sasa wajibu wetu kama chadema ni kuwa sauti ya wote wanaoumizwa kwenye nchi hii”
Akizungumzia kuhusu wanachama walioamua kurudi kwenye chama chao, Heche amesema kuwa wanawapokea kwani waligundua kuwa wamekosea na ndio maana wamerudi mara baada ya kujitathmini.

Aidha amewataka wananchi kuja kwa wingi katika mkutano wanaotarajia kuufanya katika uwanja wa mwembetogwa kwani wana mengi ya kuwaambia wananchi wa Mkoa wa Iringa.
Kwa upande wake Katibu wa Chadema Mkoa wa Iringa Leonard Kurwijilla amesema kuwa Ujio wa heche Mkoani hapa utatoa tafsiri ya kisiasa huku akiwataka wananchama wao kuendelea kuungana kwa kila jambo.
