PDF yatekeleza mradi wa kisima cha maji Ihongole
10 August 2026, 09:31

Na Fredrick Siwale
Shirika la People Development Forum (PDF), kwa kushirikiana na Serikali, limeanza kutekeleza mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji katika Mtaa wa Ihongole, uliopo Kata ya Boma, Halmashauri ya Mji Mafinga.
Akizungumza mara baada ya kuanza kwa uchimbaji wa kisima hicho katika Shule ya Msingi Mwongozo, iliyopo Mtaa wa Ihongole, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Festo Atanas Madenge, amesema mradi huo utasaidia wananchi wanaozunguka shule hiyo kupata huduma ya maji safi na salama.
Aidha, amewataka wananchi wa mtaa huo kujiandaa kuunganishiwa huduma ya maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MAUWASA), kwani kutakuwa na vituo vitakavyowezesha usambazaji wa maji hadi majumbani.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwongozo amelishukuru Shirika la PDF kwa kuwapatia huduma hiyo ya maji, sambamba na kujenga vyoo 40 vya mashimo, hatua ambayo amesema itasaidia kuimarisha afya na ustawi wa wanafunzi shuleni hapo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Ihongole wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo, wakisema utawasaidia kupata huduma ya maji ambayo wamekuwa wakiikosa kwa muda mrefu.
Nao wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwongozo wameishukuru Serikali kwa kuwakaribishia huduma ya maji ya kisima, wakisema awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji, hali ambayo ilikuwa ikiathiri masomo yao.
