Kenan awaita Chadema kwenye mdahalo
19 June 2026, 08:16

“Tujadiliane na tujenge nchi yetu kwa upendo, siyo kujenga nchi kwa kuibomoa,”
Na Hafidh Ally
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Kenani Laban Kihongosi, amewataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukubali kufanya naye mdahalo wa wazi kuhusu misimamo na sera za vyama vyao.
Kihongosi ametoa wito huo mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na wanachama na wananchi wakati wa ziara yake ya kikazi na kuongeza kuwa mdahalo huo utasaidia wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu tofauti za kisera na mipango ya maendeleo inayopendekezwa na vyama hivyo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika katika Viwanja vya Ruaha Sokoine, Kata ya Ruaha Mbuyuni, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, amesisitiza kuwa wanasiasa wanapaswa kufanya siasa za kistaarabu na si siasa za kutafuta umaarufu.
Aidha, amesema yuko tayari kushiriki mdahalo wa wazi kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa na maendeleo, akieleza kuwa hoja zinapaswa kujibiwa kwa hoja katika mazingira ya kuheshimiana.