Nuru FM

Dc Moyo aagiza kukamatwa wazazi watakaowaozesha wanafunzi

3 September 2021, 9:21 am

Iringa

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Wilaya ya Iringa ameagiza kuwafikisha Mahakamani wazazi watakaobainika kuwashawishi watoto Wao kufeli kwa makusudi mitihani ya kuhitimu darasa la Saba kwa lengo la kuwaozesha na ama kwenda kuwatumikisha katika kazi za ndani nje ya Wilaya hiyo.

Akizungumza Kwenye ziara ya kusikiliza kero za Wananchi katika Tarafa ya iliyopewa jina la ULIPO NIPO TOA KERO YAKO TUIPATIE MAJAWABU SEMA UKWELI NA SIYO MAJUNGU,  Mh. Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa kumekuwa na tabia ya Wananchi kukatisha ndoto za watoto kwa kuwashinikiza watoto wa kike kuolewa badala ya kuendelea na masomo kutokana na tamaa ya fedha inayowakabili.

Mkuu wa Wilaya amewaagiza viongozi wa vijiji na kata Wilayani humo kufanya sensa ya watoto watakaoanza mitihani ya kuhitimu darasa la Saba  mwaka huu na kufuatilia mwendo wao Kabla na baada ya kuhitimu lengo likiwa ni kupata Taarifa sahihi zinazowahusu Ili kuwalinda wasiozeshwe ama kurubuniwa kwenda kufanya kazi za ndani katika maeneo mbalimbali ya Miji.

Moyo alisema kuwa watoto wa kike wanahaki ya kusoma na kuzifikia ndoto zao kama ilivyokuwa kwa wanawake wengine wenye mafanikio makubwa dunia kwa kuwa walifanikiwa kuiishi ndoto yao
kutokana na wazazi kuwakuza kwenye malezi bora.

Wakiongea kwenye mikutano ya hadhara inayongozwa na mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo wananchi hao walisema kuwa kumekuwa na tabia ya wazazi kuwakatisha masomo kwa makusudi watoto wao kwa tama ya fedha kidogo ambazo zimekuwa zikiua ndoto za watoto hao.