Nuru FM

Serikali Yatoa Bilioni 2.5 Kukamilisha Ujenzi Wa Soko La Machinga Complex Dodoma

29 March 2022, 1:22 pm

SERIKALI imetoa Sh.Bilioni 2.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa soko la wazi la Machinga jijini Dodoma lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 4,000.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba ameyasema wakati akizungumza na Machinga wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo.

Alisema ili kufanikisha ujenzi wa mradi huo kukamilika kwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha fedha hizo ili kupatia eneo la uhakika la kufanyia biashara zao wafanyabiashara hao.

“Mradi huu utawasaidia kupanda juu kimapato lakini pia ni eneo lenye usalama kwa ajili ya biashara zenu hivyo hata taasisi za kifedha zinaweza kuwapatia mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji yenu kwakuwa mpo katika eneo rasmi sasa,”alisisitiza Nchemba.

Aidha, alisema ili mradi huo usikwame Rais ametoa kiasi hicho cha fedha ili kutimiza malengo ambayo walikuwa wamejiwekea ya kuwapanga machinga katika maeneo rasmi.

“Rais ameagiza fedha zitolewe bila kuchelewa hivyo nawaalika timu ya Mkoa kuja ofisi na mchanganuo wao wa fedha zitakavyotumika na mara baada ya mradi huu kukalimilika atakuja mwenyewe kuushuhudia,”alisema.

Kwa upande wake MKUU wa Mkoa wa Dodoma ,Anthony Mtaka,amesema kuwa katika soko hilo kutakuwa na huduma mbalimbali za kijamii hususani Msikiti pamoja na Kanisani.

”Hili soko litkapokamilika litakuwa na huduma mbalimbali za kijamii watu ambao watataka kusali kutakuwa na Msikiti na Kanisa na pia kutakuwa na sehemu maalum ya akina mama kunyonyeshea watoto wao wakati wakitekeleza majukumu yao”amesema Mtaka
Aidha amesema kuwa eneo hilo pia kutakuwa na Baa ya kupata vinywaji mbalimbali na litafungiwa CCTV Camera kwa ajili ya usalama wa mali zao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, alimshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha fedha hizo ili kuhakikisha Machinga wanafanya shughuli zao kwenye maeneo rasmi.

“Tunamshukuru sana Rais kwa kiasi hichi cha fedha ambacho kinakwenda kutoa majibu kwa machinga wetu ambao wamekuwa wakipata shida kwa muda mrefu kwa kukosa eneo rasmi kwa ajili ya kufanya biasahra zao,”alisema.

Pia, alisema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia wajasiriamali wadogo zaidi ya 4,000.

Naye Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi alisema kukamilika kwa mradi huo kutawaondolea adha nyingi walizokuwa wakizipata ikiwemo mvua na jua.

“Mheshimiwa Waziri sisi Machinga mradi huu tunausubiri kwa hamu sana kwa kuwa unakwenda kujibu kero zetu ambazo tumekabiliana nazo kwa muda mrefu lakini pia utatuwezesha kuaminika na taasisi za fedha kupata mikopo kwa ajili ya mitaji,”alisisitiza Mponzi.