Nuru FM

Mradi wa SLR waanza kuleta matokeo Iringa

1 March 2024, 12:13 pm

Wananchi waliofikiwa na Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR). Picha na Frank Leornad

Na Frank Leornad

WANANCHI waliofikiwa na Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bioanuai (SLR) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wameanza kuitumia elimu wanayopatiwa katika mashamba darasa wilayani Iringa, kuifanya kuwa endelevu ili kuwakwamua kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa mradi wa ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa unaosimamiwa na SLR wa kata ya Nzihi wamemueleza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga jinsi mradi ulivyo na tija kwao na kuweza kuwainua kiuchumi kijijini hapo.

“Sisi kikundi chetu kilianza mwaka 2023 tukiwa na ng’ombe watatu. Ng’ombe hao walizaa madume matatu na hivi sasa wana mimba tena. Tunatarajia hadi mwezi wa tano mwaka huu wote watakuwa wamezaa tena,” alisema Jackson Kasike Mwenyekiti wa kikundi cha Agape.

Kasike alisema zaidi ya wanavijiji 20 waliofika hapo kujifunza kwasasa wana ng’ombe wao ambao tayari wanatoa maziwa na kuongeza uchumi katika ngazi ya familia.

Kwa kupitia ziara ya kamati ya usimamizi wa SLR ya kukagua shughuli zilizotekelezwa katika kata hiyo ya Nzihi, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais amewahimiza maafisa viungo wa halmashauri zinazotekeleza mradi huo wa SLR kuitisha mikutano ya mara kwa mara na Kamati za Maliasili na Mazingira za Vijiji ili kuendelea kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

“Wanakikundi mnaoneka mna mwamko mkubwa. Tunataka kuona matunda ya mashamba darasa haya, sitaki kusikia mradi huu unapo maliza muda wake na kila kitu kinaishia hapa, tunataka kuona tija endelevu ya mradi huu,” alisisitiza Maganga.

Aidha Maganga aliwaomba wananchi waliozungukwa na mradi huo kutoa ushirikiano wa kutosha katika uhifadhi wa mazingira na urejeshwaji wa uoto wa asili.

“Ndugu zangu serikali ilianzisha mradi huu mahsusi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki na mazingira ikiwamo ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji hivyo kila mmoja wetu ni lazima awe mlinzi wa kwanza wa mazingira,” alisema.

Kata ya Nzihi ina jumla ya miradi mitano inayotekelezwa na SLR ukiwamo mradi wa hifadhi ya misitu uliopo kijiji cha Ilalasimba na Magubike, shamba darasa la kilimo cha mazao, shamba darasa la malisho ya mifugo, na mradi wa ufugaji wa Ng’ombe wa maziwa.

Maganga alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali kubwa ya maliasili za misitu, nyika, ardhi oevu, maziwa, mito na bahari ambavyo ni msingi wa utajiri wa maliasili.

“Tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza jamii zetu umuhimu wa kukabiliana na uharibifu wa mazingira. Mradi huu unatoa mafunzo kwa wakulima na wafugali kuhusu mbinu mbalimbali za uendeshaji shughuli za kilimo na ufugaji ambazo ni rafiki kwa utunzaji wa mazingira,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Muhoja alizungumzia madhara ya uharibifu wa uoto wa asili ikiwemo ukataji wa miti sambamba na mabadiliko ya tabianchi akisema yanaonekana wazi katika maeneo mengi ya halmashauri yake.

Muhoja alisema kamati za maliasili na mazingira za vijiji ambazo zimeanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1987 ni nguzo muhimu katika urejeshaji wa uoto wa asili na hifadhi za bianuai kwani kamati hizo ndizo zilizopewa mamlaka ya kusimamia masuala ya maliasili na mazingira katika maeneo ya vijiji.

Mradi wa SLR unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 25.8 unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitano unaotarajia kukamilika mwaka 2025 ulioanza mwaka 2021 ukihusisha jumla ya Mikoa mitano, Halmashauri saba, Kata 18 na vijiji 54.

Halmashauri zinazonufaika na mradi huo ni Iringa Vijijini (Iringa), Wilaya ya Mbeya na Mbarali (Mbeya), Halmashauri za Sumbawanga vijijini (Rukwa) pamoja na Halmashauri za Wilaya za Tanganyika na Mpimbwe (Katavi).