Nuru FM

Uvccm Iringa wapongeza kurejeshwa kwa mikopo ya asilimia 10

19 April 2024, 11:06 am

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Agrey Tonga akizungumzia kuhusu MIKOPO ya asilimia 10 iliyorejeshwa na Rais Samia. Picha na Adelphina Kutika

Mikopo ya asilimia 10 inawanufaisha vijana, Wanawake na watu wenye ulemavu katika shughuli za kiuchumi.

Na Adelphina Kutika

Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassani kwa kurejesha tena utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika halmashauri zote nchini kuanzia Julai, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa Habari  ofisini kwake, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa  AGREY TONGA   ametoa pongezi na shukrani hizo kwa Rais Samia baada ya Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kutoa taarifa hiyo bungeni Dodoma, April 16, 2024, wakati akitoa hotuba kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.

“Kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kusanifu na kujenga mfumo mpya unaoitwa Wezesha Portal utakaotumika kwa ajili ya taratibu za ukopeshwaji wa vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu, mfumo huu utaondoa changamoto za mfumo zilizokuwepo awali kabla ya mikopo kusimamishwa, maboresho mengine ni kujenga uwezo kwa Wasimamizi wa mikopo hiyo kwa kuongeza idadi ya Wasimamizi wa mikopo kwenye ngazi ya kata ambapo maafisa maendeleo ya jamii 787 wameajiriwa na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu.

Amebainisha kuwa Utaratibu ulioboreshwa unahusisha uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Mwenyekiti huyo amesema mikopo inayotarajiwa kutolewa ni shilingi bilioni 227.96 ambapo shilingi bilioni 63.67 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa.

Amesema kuwa shilingi bilioni 63.24 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na shilingi bilioni 101.05 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25

MWISHO