Nuru FM

Mfumo wa alama za vidole kwa WAVIU wazinduliwa hospitali ya rufaa Iringa

16 November 2023, 8:34 pm

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Craig Hart akipokea malekekezo kuhusu mfumo huo. Picha na Godfrey Mengele.

Na Godfrey Mengele.

Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa imezindua mfumo  wa uandikishaji kwa alama za vidole lengo likiwa kuimarisha huduma kwa watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) ili kupata takwimu sahihi za wale wanaoishi na maambuzi hayo pamoja na wale watakaotambulika.

Mfumo huu umefadhiliwa na USAID na kuzinduliwa na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Craig Hart, katika kusherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwa ufadhili wa dawa za ARVs kutoka Marekani.

Katika hotuba yake Craig amesema kuwa mfumo huo unakusudia kuleta mabadiliko chanya kwa WAVIU kwa kutoa huduma bora zaidi na kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa.

Craig Amesema “..katika kusheherekea miaka 20 hii ameona nia ya dhati na utelezwaji mzuri wa miradi inavyowafikia walengwa hivyo shirika hilo litaendelea kufadhili miradi inayolenga kuboresha maisha ya watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na utatuzi wa changamoto nyingine..”

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Iringa, Dr. Mohamed Mang’una amesema kuwa katika sekta ya afya mkoani iringa ni mengi yamefanya kupitia ufadhili wa USAID kwani kwa sasa kumeshuhudiwa idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kupima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutokana na ukaribu wa vituo vya kutolea huduma hiyo katika maeneo tofauti tofauti mkoani hapa

Sauti ya Mganga Mkuu Mkoa wa Iringa Dr. Mang’una

“.. kwa sasa kuna ongezeko la vituo vya kutoa huduma kwa WAVIU kutoka 8 hadi 261 vinavyofadhiliwa na USAID kufikia 136 hivyo tunapata idadi kubwa ya wateja wanaopata huduma hii ambapo ni zaidi ya elfu 80 na wanaotumia dawa za ARVs wakifikia asilimia 90..” Dr Mang’una

Kupitia kuzinduliwa kwa mfumo huu Mganga Mkuu wa Iringa, Dr. Mohamed Mang’una amesema kwa sasa kutakuwa na urahisi wa kupata takwimu sahihi za WAVIU kwani awali walikuwa wanashindwa kupata takwimu hizo si kwa wenye maambukizi mapya wala hawa wa sasa waliogundilika au watakao gundulika kuwa na maambukizi ambapo hata ufuatiliaji ulikuwa mgumu kuwapata hata wanaoacha matumizi ya dawa.

Mfumo huu unazinduliwa kwa mara ya kwanza Mkoani Iringa ikitajwa hatua yenye nia madhubuti ya kupata idadi sahihi ya WAVIU pamoja na kuirahisishia serikali na wadau wake ikiwamo USAID katika kuendelea kupambana na maambuziki mapya kwani mgonjwa atakapo jiandikisha katika kituo kimoja taarifa zake hazitajirudia katika kituo kingine tofauti na hapo awali.