Nuru FM

Uzalishaji wa sukari umeongezeka hapa Nchini

22 January 2023, 10:45 am

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema kuwa uzalishaji wa sukari nchini umeongezeka hadi kufikia zaidi ya tani 70,000 na kufanya kuwa na zaidi ya tani 160,000 kwenye maghala katika kipindi cha 2022 /2023 na kupunguza kwa kiasi kikibwa uhaba wa sukari nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji katika kikao na wadau wa uzalishaji wa sukari chini kilicholenga kufahamu hali ya uzalishaji wa sukari nchini, Dkt. Abdalah amesema Serikali inaendelea kuhakikisha uwepo wa uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo Ili kuleta tija kwa Taifa zima.

Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na biashara Dkt. Hashil Abdalah akizungumza katika kikao na wadau wa uzalishaji wa sukari chini kilicholenga kufahamu hali ya uzalishaji wa sukari nchini kilichofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi za TIC Jijini Dar es salaam

“Mwaka huu tumeingiza uzalishaji wa sukari wa kiwanda kipya cha bagamoyo ambao umepelekea uzalishaji wa sukari kwa ujumla wake kuongezeka kuliko hata ule wa mwaka jana, hii inapelekea mazungumzo haya kuendelea mara kwa mara” Ameongeza.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo ya kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari ni kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikari ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani katika kuhamasisha uzalishaji na uwekezaji kwenye Sekta hiyo.

“Rais Samia mara kadhaa amekuwa akiweka wazi kuwa Tanzania inawahitaji wawekezaji katika Sekta mbalimbali na yeye mwenyewe kusimamia kwa vitendo kuhakikisha wawekezaji wanaongezeka” ameeleza Dkt. Abdallah

Aidha amewahakikishia wakulima wa zao la miwa kuwa sasa changamoto zao za kupata masoko zimepata ufumbuzi kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa sukari.

Kwa upande Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Sukari Tanzania, Seif. A. Seif, amesema kuwa ongezeko kubwa la sukari linaonesha nchi ina sukari ya kutosha hivyo imekuwa faraja kubwa kwa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani alikuwa na azma ya kutaka nchi ijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gungu Mibavu, amesema kutokana na ongezeko la uzalishaji wa sukari nchini, inaonesha kwamba jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhamasisha uzalishaji na uwekezaji kwenye tasnia hiyo unazaa matunda.