Nuru FM

REA yafanikisha utekelezaji mradi wa Umeme Kilolo

24 September 2023, 6:08 pm

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage, Mwenyekiti wa Kijiji cha Idete, Henry Lekuti na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Lung’ali Natural Resources, Padre Luciano Mpoma wakijadili jambo wakati wakikagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa umeme wa maji (kilovoti 2400).

Mkurugenzi waTeknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala, Wakala wa Nishati Vijijini – REA, Mhandisi Advera Mwijage umesema atahakikisha washirikiana na Sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na nishati ya uhakika vijijini.

Mhandisi Mwijage ameyasema hayo baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa
umeme wa maji (kilovoti 2400), wa Idete Wilayani Kilolo unaotekelezwa na Kampuni ya Lung’ali
Natural Resources Co ltd.

Amesema, hadi kufikia sasa REA mpaka imetoa ruzuku ya Shilingi 4 Bilioni kwa mradi huo
ulio chini ya Kanisa Katoliki Mkoa wa Iringa, ambazo zimetumika kwa utafiti wa mazingira, ujenzi wa Bomba la Maji na Jengo lenye mtambo wa kuzalishia umeme, (Power House).

“REA inafanya kazi na sekta binafsi ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora ya Nishati Vijijini na kuchangia katika shughuli za uchumi zinazoongeza kipato kwa Wananchi. Serikali haiwezi kufanya kila kitu katika miradi ya maendeleo inayogusa wananchi.” alisema Mhandisi Mwijage.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni inayozalisha umeme wa Maji ya Lung’ali Natural Resources, Padre Luciano Mpoma alisema wanatarajia kuanza uzalishaji wa umeme Januari 2024 na kudai kuwa ujenzi unaendelea vizuri na utawasaidia Wananchi wa Idete na maeneo mengine kuwa na umeme wa uhakika.

Naye Mwenyekiti wa Kata ya Idete, Henry Kikoti ameelezea shauku ya Wananchi kwamba wanataka mradi huo ukamilike, kwani watakuwa na umeme wa uhakika kutokana na uliopo kutotosheleza kufanikisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi na uwekezaji.