Nuru FM

Dc Moyo kuwachukulia hatua kali za kisheria watakao haribu vyanzo vya maji.

24 March 2022, 5:44 am

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo kuwachukulia hatua Kali za kisheria wananchi na viongozi wote watakao hatibu vyanzo vya Maji na kukata hovyo miti.

Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya maji wilaya ya Iringa yaliyofanyika katika Kijiji Cha magunga alipokuwa akishilikiana kupanda zaidi ya miti Mia tano ambayo ni rafiki ya maji.

Moyo alisema Kuwa Serikali imekuwa inatumia gharama kubwa kuhifadhi vyanzo vya maji na kuwapelekea maji Wananchi Lakini Wananchi wamekuwa wakiharibu vyanzo vya maji kwa makusudi bila kujali Serikali imetumia gharama kiasi gani.

Alisema kuwa maadhimisho ya wiki ya maji ya mwaka huu 2022 ambayo yameanza rasmi tarehe 16/03/2022 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22/03/2022 lengo kubwa ni kukumbushakutunza rasmali za maji ni maisha ya wanadamu wote.

Moyo  alisema kuwa wilaya ya Iringa inaendelea kutoa huduma ya maji safi na salama kwa maeneo yote ya vijijini kwa wastani wa asilimia 75.6 na Iringa mjini imefikia asilimia 97 na hayo yote yanaendelea kuboreshwa zaidi na mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan.

Alisema kuwa mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan anatambua adha ambayo wananchi wanaipata hasa wanawake kwenda kufuata maji umbali mrefu na kusababisha kero nyingi kwenye familia.

Moyo alisema katika mwaka wa fedha wa 2021/2122 wilaya ya Iringa inaendelea kukarabati miradi mbalimbali ya maji ikiwepo ya vijiji vya Nyabula/Ulanda,Magunga/Itengulinyi,Makatapola,Mbweleli,na Makuka yote kwa lengo la kuhakikisha wanawatua ndoa wakinamama wa wilaya hiyo.

Alisema kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suruhu Hassan amefanikiwa kupata fedha na kuanza kutekeleza miradi mingine zaidi kupitia Mpango wa Maendeleo ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko -19 ambayo imeanza kutekelezwa katika majimbo ya Kalenga na Isimani.

Moyo alisema kuwa katika wilaya ya Iringa wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaendelea kuvilinda vyanzo vya maji na kupanda mti ambayo inasaidia kutunza maji yaliyopo ardhini kwa ajili ya matumizi.

Alisema kuwa wataendelea kuitumia kauli mbiu ya maazimisho ya maji mwaka huu inayosema kuwa “maji chini ya ardhi,hazina isiyoonekana kwa maendeleo endelevu” kwa kvitunza vyanzo vyote ya maji vilivyopo wilaya ya Iringa.

Kwa upande wake meneja wa RUWASA wilaya ya Iringa Eng Masoud Samila alisema kuwa katika maadhimisho ya siku ya maji wilaya ya Iringa yaliyofanyika katika Kijiji Cha magunga wamefanikiwa kupanda jumla ya miti mia tano (500) ambayo ni rafiki na maji.

Eng Samila alisema kuwa lengo la serikali kuhakikisha inamtua ndoo mama kichwani na kuwasaidia wananchi wa wilaya ya Iringa kupata maji safi na salama kwa ukaribu ambao utasaidia kuendelea kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.