Nuru FM

RC Serukamba: Taasisi za umma jiungeni na mfumo wa ‘NeST’

14 May 2024, 7:50 pm

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Peter Serukamba akiwa katika Picha ya pamoja baada ya kutoa maagizo kutumia mfumo wa “NeST“. Picha na Godfrey Mengele

Mfumo mpya wa manunuzi utakuwa chachu ya kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pindi wanapofanya manunuzi ya mali za umma.

Na Godfrey Mengele

Mkuu wa Mkoa wa Iringa ,Peter Serukamba ameziagiza Taasisi za umma Mkoani Iringa ambazo hazijaanza kutumia mfumo mpya wa manunuzi wa kielectronic “NeST” uliochini ya  Mamlaka ya udhibiti ya ununuzi wa umma (PPRA) Tanzania zianze mara moja ili kudhibiti mianya ya rushwa.

Serukamba ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe na Wakurugenzi wa bodi ya Mamlaka ya udhibiti ya ununuzi wa umma PPRA yanayofanyika Mkoani Iringa na kuzitaka taasisi hizo kuzingatia maagizo ya serikali kuhakikisha wanachakata manunuzi kwa kutumia mfumo huo.

Sauti ya Serukamba

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike amesema baada ya kufanya ukaguzi, wamejiridhisha na maendeleo ya mfumo wa huo na tayari baadhi ya taasisi zimeanza kuutumia huku wakiendelea kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa matumizi yake.

Sauti ya Mwenyekiti Bodi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya udhibiti ya ununuzi wa umma (PPRA), Eliakim Maswi amesema mpaka sasa mfumo huo umefanikiwa kusajili taasisi 1,143 nchini huku rasmi sheria mpya ya ununuzi inayozitaka taasisi kutumia mfumo huo itaanza kutumika julai mosi hivyo kwa taasisi zisizotumia zitakumbana na mkono wa sheria.

Sauti ya Mkurugenzi

Mfumo huu mpya wa manunuzi wa kielectronic “NeST” unajengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na serikali na umeunganishwa na mifumo 18 ya serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza muda na gharama za michakato ya manunuzi, kudhibiti vitendo vya udanganyifu, rushwa na kuzuia ukosefu wa maadili.

MWISHO