Nuru FM
Nuru FM
8 August 2024, 14:22

Na Frank Leonard, Iringa
Watia nia wa ubunge katika baadhi ya majimbo ya mkoa wa Iringa wametuhumiwa kuomba ongezeko la misiba ili kujipatia umaarufu na kuonyesha kujali jamii.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas, alitoa taarifa hiyo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Iringa Vijijini katika muendelezo wa vikao vyake na halmashauri za CCM za wilaya zote mkoani Iringa.
Asas alieleza kuwa baadhi ya watia nia wamekuwa wakiulizia misiba na kushiriki kila msiba katika majimbo wanayotaka kugombea, wakitoa misaada ya kifedha ili kujiongezea umaarufu.
Alikosoa tabia hii, akisema ni siasa chafu inayotumia huzuni za watu kwa faida za kisiasa badala ya kuonyesha huruma ya kweli.
Alionya kuwa vitendo hivi vinaweza kuharibu maadili ya kijamii na kudhoofisha demokrasia.
Asas alisema CCM imejipanga kuhakikisha wagombea wake wanazingatia maadili na kanuni, na chama kitachukua hatua kali kwa wale watakaovunja kanuni hizo.
Pia, Asas alikabidhi simu janja 150 kwa CCM Iringa Vijijini ili zitumike kusaidia usajili wa wanachama kidigitali, akisisitiza umuhimu wa wanachama wote kusajiliwa ili kuimarisha nguvu ya chama katika uchaguzi.
Mwisho.