Nuru FM

Maonesho ya Nanenane kufungua fursa Iringa

17 July 2026, 09:26

Maonesho hayo, yanayofanyika kwa mara ya kwanza kwa ngazi ya mkoa, yanatajwa kuwa hatua muhimu ya kusogeza huduma karibu na wakulima, wafugaji na wavuvi, badala ya kulazimika kusafiri umbali mrefu kuhudhuria maonesho ya kanda.

Na Hafidh Ally

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amewataka wananchi kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbegu bora, kilimo cha kisasa, umwagiliaji, matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na huduma bora za ugani kuanzia uzalishaji, uvunaji, uhifadhi hadi uchakataji wa mazao.

Mhe. Kheri ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Nanenane ngazi ya Mkoa wa Iringa yaliyofanyika katika Viwanja vya Kihesa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambapo amesema kuwa sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa mkoa, hivyo ni muhimu wakulima wakatumia teknolojia na mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kipato.

Sauti ya RC

Aidha RC Kheri amesema changamoto bado ipo kwa baadhi ya wakulima kuzalisha bila kuzingatia mahitaji ya soko, jambo linalosababisha kushuka kwa bei na kupunguza faida ya uzalishaji.

Sauti ya RC

Alisema maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kutegemea kuongeza uzalishaji pekee, bali yanahitaji matumizi ya mbegu bora, pembejeo sahihi, teknolojia za kisasa, umwagiliaji, ubunifu, uwekezaji na ushirikiano wa wadau ili kuongeza tija na thamani ya mazao.

Kheri alisema Iringa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutokana na ardhi yenye rutuba, hali nzuri ya hewa na rasilimali za maji kwani mwaka 2023 mkoa ulizalisha zaidi ya tani milioni moja za mazao ya chakula na tani 137,888 za mazao ya biashara.

Awali Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayeshughulikia Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Elias Luvanda, na Mstahiki Meya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada  wamesema jumla washiriki 87 wanashiriki maonesho hayo, zikiwemo halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, taasisi za utafiti, kampuni za mbegu na pembejeo, taasisi za fedha, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Sauti ya Luvanda vs Meya

Mratibu wa Kitengo cha Uhamishaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Iringa, Bi. Lilian Ngusi, amewashauri wakulima kuzingatia matumizi ya mbegu bora na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Sauti ya Mratibu Tari

Ngusi alisema miongoni mwa teknolojia zilizovutia wageni ni mbegu bora za viazi mviringo, viazi lishe, maharage, soya na miche bora ya parachichi, pamoja na bidhaa mbalimbali zilizoongezwa thamani ili kuonesha namna mazao yanavyoweza kuleta faida kubwa zaidi kuliko kuuzwa yakiwa ghafi.

Alifafanua kuwa kwa zao la viazi mviringo, TARI inawahimiza wakulima kuingia kwenye uchakataji kwa kuzalisha bidhaa kama chipsi, hatua inayoweza kuongeza thamani ya mazao na mapato ya kaya.

Maonesho ya Nanenane yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” yakilenga kuhamasisha wakulima, wafugaji na wadau wa sekta ya kilimo kuongeza uzalishaji wenye tija, kuzalisha kwa kuzingatia mahitaji ya soko na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya Taifa ifikapo mwaka 2050.