Wanafunzi Mlamke waonywa matumizi ya bangi kali
28 May 2026, 13:15

Elimu ya rika balehe iliyotolewa itasaidia kupunguza tatizo la matumizi ya sigala kali na bangi kwa wasichana wanaosoma katika shule ya Mlamke.
Na Adelphina Kutika
Wasichana wa Shule ya Sekondari Mlamke mkoani Iringa wametakiwa kuacha matumizi ya bangi, sigara kali pamoja na kujiepusha na makundi mabaya yanayoweza kuharibu maisha na ndoto zao za baadaye.
Wito huo umetolewa na A/Insp. Magret Laizer pamoja na Inspekta Lidya Sospeter kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kata ya Ilala/Makorongoni, Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Iringa, na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na kuwahimiza wanafunzi wa kike kujitambua, kuzingatia maadili mema na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya kielimu na kijamii.
Kwa upande wao, viongozi wa dini akiwemo Mlezi wa baraza kuu la wanawake wa Kiislamu mkoa wa Iringa Bi Halima Issa Abdullahi na Mchungaji Ester Magava wameitaka jamii pamoja na wazazi kuhakikisha malezi bora yanaendelea kutolewa kwa watoto ili kujenga kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu.
Naye Mwandishi Mchechemuzi wa habari za watoto mkoani Iringa Tukuswiga Mwaisumbe amewataka wanafunzi hao kujiepusha na ushawishi wa makundi mabaya hasa katika kipindi cha balehe na badala yake kuzingatia masomo yao na kutafuta ushauri kwa walimu wa malezi wanapokutana na changamoto.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Aneth Mponzi wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa madhara ya matumizi ya bangi, sigara pamoja na kujiingiza katika vitendo visivyofaa katika umri mdogo.
