Nuru FM

Wajane Iringa waomba kuwezeshwa kiuchumi

24 June 2026, 09:27

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akizungumza katika maandhimisho ya siku ya wajane. Picha na Joyce Buganda

Na Joyce Buganda

Serikali Imeshauriwa kuongeza juhudi za kuwawezesha wajane na wagane kupata haki zao kwa wakati, hususan katika masuala ya mirathi na uwezeshaji wa kiuchumi baada ya kufiwa na wenza wao.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wajane yaliyofanyika kimkoa Juni 23, 2026 katika Shule ya Sekondari Kilolo, wilayani Kilolo, Afisa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la SOS Children’s Villages, Bi. Jesca Kawonga, alisema kuna umuhimu wa Serikali kutoa kipaumbele kwa wajane na wagane kwa kuwasaidia kupata mirathi kwa haraka pamoja na kuwawezesha kupata mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuendelea kuhudumia familia zao.

Sauti Jesca

Bi. Kawonga alisema shirika hilo lilishiriki maadhimisho hayo kwa kutoa mada mbalimbali zilizolenga kuhamasisha malezi na makuzi bora ya watoto kuanzia utotoni hadi balehe, afya ya uzazi pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi.

Nao Baadhi ya wajane na wagane waliohudhuria maadhimisho hayo waliiomba Serikali kuharakisha upatikanaji wa haki za mirathi, wakieleza kuwa wamekuwa wakitumia muda mrefu mahakamani kufuatilia haki na mali walizoachiwa na wenza wao.

Sauti Wajane

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mh. Kheri James, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, amewataka wajane na wagane kujenga utamaduni wa kutenganisha mali za familia na mali za ndugu ili kuepusha migogoro na changamoto zinazoweza kujitokeza pindi mmoja wa wanandoa anapofariki dunia.

Sauti ya Kheri

Katika hatua nyingine, Mhe. Kheri amehimiza wanandoa kuhakikisha ndoa zao zinatambulika kisheria na kuwa wazi kuhusu mali na rasilimali wanazomiliki kwa pamoja ili kuzuia migogoro na upotevu wa mali baada ya kifo cha mmoja wao akibainisha kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Iringa una wajane 53,374 sawa na asilimia 7.4 ya wakazi wote wa mkoa huo, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya haki za wajane na kuimarisha ulinzi wa makundi hayo muhimu katika jamii.

Maadhimisho ya Siku ya Wajane mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo: “Imarisha Haki, Utu na Uwezeshaji wa Kiuchumi.”