Ugute walalamika mwekezaji kupewa hekta 400 za ardhi kimyakimya
22 July 2026, 09:01

Wananchi wa Kijiji cha Ugute wametaka mchakato wa kupatikana kwa mwekezaji kuwekeza kijijini kwao usitishwe ili washirikishwe.
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa Kijiji cha Ugute, Kata ya Isalavanu, Halmashauri ya Mji Mafinga, wamelalamikia uamuzi wa uongozi wa kijiji hicho wa kumpatia mwekezaji zaidi ya hekta 400 za ardhi, wakidai mchakato huo umefanyika bila ushirikishwaji wa wananchi.
Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, wananchi hao walisema hawatambui uhalali wa uamuzi huo kwa kuwa hawakushirikishwa ipasavyo katika hatua za kumpatia mwekezaji eneo hilo.
Aidha, walisema hawajapewa taarifa kuhusu aina ya uwekezaji unaotarajiwa kufanyika, muda wa uwekezaji huo, wala manufaa yatakayopatikana kwa kijiji, hivyo wakaitaka Serikali kusitisha mchakato huo hadi wananchi watakapopewa taarifa na kushirikishwa kikamilifu.

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ugute, Sadick Vincent Mpwapwa, alisema uongozi wa kijiji ulifanya mikutano mitatu ya wananchi kujadili suala hilo baada ya kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa Halmashauri ya Mji Mafinga.
Alieleza kuwa katika makubaliano hayo, kijiji kiliweka masharti kwa mwekezaji ikiwemo kuweka shilingi milioni 30 kwenye akaunti ya kijiji, kujenga nyumba mbili za watumishi pamoja na kuchimba visima vitano vya maji, masharti ambayo alisema mwekezaji alikubali kuyatekeleza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Mheshimiwa Dickson Lutevele Villa, alisema endapo itathibitika kuwa mwekezaji alifuata taratibu zote za kisheria na wananchi walitoa ridhaa kupitia mikutano halali ya kijiji, atauunga mkono uwekezaji huo kwa kuwa unaweza kuchangia maendeleo ya kijiji.
