Barabara ya Ipogolo yafunguliwa rasmi baada ya matengenezo
15 October 2026, 09:49

Barabara hiyo ni kiungo muhimu cha usafirishaji na biashara kinachochangia kuunganisha mataifa mbalimbali kupitia mtandao wa barabara za kikanda na kimataifa.
Na Chacha Robert
Barabara ya Ipogolo mkoani Iringa imefunguliwa rasmi baada ya kufungwa kwa takribani mwezi mmoja kupisha matengenezo ya daraja na upanuzi wa mtaro wa Mto Ruaha, hatua inayolenga kupunguza athari za mafuriko wakati wa msimu wa mvua.
Akikagua mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema barabara hiyo ni muhimu kwa usafiri na uchumi kutokana na matumizi yake na magari ya mizigo, abiria na wananchi kwa ujumla ambapo kufungwa kwake kulilenga kuimarisha usalama wa watumiaji na kuzuia kukatika kwa barabara hiyo kutokana na mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko.
James amewataka wananchi kushirikiana katika kulinda miundombinu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa watembea kwa miguu na madereva wa bodaboda na bajaji kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao ili kuepusha ajali.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Iringa, Michael Anyandwile, amesema matengenezo hayo yamegharimu shilingi milioni 660, yakihusisha ujenzi wa daraja na upanuzi wa mtaro ili kuruhusu maji kupita kwa usalama.
Naye Diwani wa Kata ya Ruaha, Musa Salum Mbungu, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawasaidia wananchi kurejea katika shughuli zao za kawaida na kupunguza hofu ya mafuriko yaliyokuwa yakijitokeza wakati wa mvua.
Diwani wa Kata ya Igumbilo, Jackson Chatanda, amesema kufunguliwa kwa barabara hiyo ni fursa mpya ya kiuchumi kwa wananchi na wafanyabiashara, akieleza kuwa barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Manispaa ya Iringa na maeneo jirani.
Ujenzi wa upanuzi wa mtaro huo ulianza tarehe 17 Septemba na kukamilika tarehe 12 Oktoba, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja uliokuwa umekadiriwa kwa utekelezaji wa mradi huo.
