Serikali yajenga Bweni Shule ya Lupembelwasenga
30 September 2026, 09:51

Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kata ya Lyamgungwe, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 wa kike katika Shule ya Sekondari Lupembelwasenga ili kuondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni na kupunguza mimba za utotoni.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ya kukagua miradi ya maendeleo, wananchi hao wamesema ujenzi wa bweni hilo ni hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya elimu na usalama wa wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kufika shuleni huku wakiomba kujengwa kwa bweni la wavulana.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lupembelwasenga, Mwl. Edda Kutika, amesema bweni hilo linalenga kupunguza safari ya takribani kilomita tisa kwa wanafunzi, pamoja na utoro na mimba za utotoni huku akisema kuwa mradi huo umegharimu Shilingi milioni 140 kutoka Serikali Kuu, huku wananchi wakichangia nguvu zao kwa kukusanya tripu 70 za mawe.
Nae Diwani wa Kata ya Lyamgungwe, Mhe. Alex Malangalila, ameishukuru Serikali kwa ujenzi huo huku akiomba kujengwa kwa maabara pamoja na kusogezwa kwa nguzo za umeme katika eneo la bweni. Pia amemshukuru mwananchi aliyetoa ekari 50 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameagiza bweni hilo kukamilika ifikapo Oktoba 15, 2026, akisema fedha na vifaa vipo.
Aidha, Mhe. Kheri amewataka wananchi kutunza miundombinu hiyo, akisema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha mazingira ya elimu na kwamba ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kulinda na kunufaika na miradi ya maendeleo.
