Mkandara achangia mifuko 100 ya saruji ujenzi wa kanisa la SDA Ngome
28 November 2026, 16:16

Na Hafidh Ally
Muumini na mdau wa maendeleo, Afande Elpidius Cleophace Mkandara, amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato la Ngome, lililopo Manispaa ya Iringa.
Akizungumza katika Harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa hilo, mgeni rasmi, Bi. Rehema Mwashingwa, aliyemwakilisha Afande Mkandara, amesema pamoja na mchango huo, mdau huyo ameahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa kanisa katika hatua mbalimbali za ujenzi hadi utakapokamilika.
Bi. Mwashingwa amesema ujenzi wa kanisa hilo ni jukumu la waumini na wadau wote, hivyo amewahimiza waumini kushiriki kikamilifu kwa kuchangia fedha na rasilimali nyingine ili kuwezesha kukamilika kwa jengo hilo na kupata mazingira bora ya kufanyia ibada.

Kwa upande wake, mzee wa kanisa hilo, Elitwaza Mtango, amemshukuru Afande Elpidius Cleophace Mkandara kwa mchango wa mifuko hiyo 100 ya saruji, akieleza kuwa utasaidia kusukuma mbele ujenzi ambao bado unahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali ili kukamilika.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi, mhazini wa kanisa hilo, Bw. Manase Geophrey, amesema kuwa kuanzia Agosti 24, 2026, kanisa liliunda vikosi nane vyenye jumla ya washiriki zaidi ya 100 kwa lengo la kukusanya fedha za ujenzi, ambapo hadi sasa limefanikiwa kupata shilingi milioni 5.2.

Naye Mchungaji Kalebu Dismass Bandi kutoka Mtaa wa Ilasa, Mufindi, amewahimiza waumini kuunganisha nguvu na kushiriki katika ujenzi huo ili kufanikisha kukamilika kwa kanisa na kuanza kulitumia kwa shughuli za ibada.
Kwa wadau na watu wengine wenye nia ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo, wanaweza kutuma michango yao kupitia namba ya simu 0743007775, kwa jina la Ngome SDA Church, au akaunti ya CRDB namba 015C496057800, yenye jina la Ngome SDA.
