Simba aliyezua taharuki Mufindi auawa
1 September 2026, 08:52

Simba huyo amewasababishia hasara wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kuua mifugo yao.
Na Fredrick Siwale
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kumuua simba aliyekuwa akivamia makazi ya wananchi na kuua mifugo katika Kijiji cha Mwikitila, Kata ya Ifwagi, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Akizungumza na Nuru FM, Afisa Mazingira na Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Aglibert Ngailo, amesema simba huyo aliingia katika maeneo ya makazi ya wananchi tangu Julai 18, 2026, na kusababisha taharuki katika kata za Nyololo, Matanana, Mbalamaziwa, Malangali, Maduma, Ihowanza, Ifwagi, Ikongosi, Bumilayunga na Itimbo.
Ngailo amesema katika kipindi chote ambacho simba huyo alikuwa akizunguka katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, amefanikiwa kuua jumla ya ng’ombe 12, mbuzi 17 na nguruwe 9.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Castory Boniface Masangula, amewataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea na shughuli zao za kila siku, akisema hali kwa sasa ni shwari baada ya simba huyo kuuawa.
