RC Kheri azindua kampeni ya Kupambana na Moto Mufindi
22 September 2026, 10:57

Na Hafidh Ally
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, kwa kushirikiana na Mradi wa FORLAND, amezindua kampeni maalumu ya kuhamasisha, kuelimisha na kuwakumbusha wananchi kuhusu madhara ya moto na umuhimu wa kulinda misitu katika Mkoa wa Iringa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Kampeni hiyo yenye kaulimbiu, “Misitu Yetu, Uchumi Wetu, Tusichome Moto Hovyo,” katika Kijiji cha Kidete, Kata ya Mdabulo, Wilaya ya Mufindi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amesema kuwa lengo ni kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kuzuia na kutokomeza matumizi yasiyokuwa sahihi ya moto yanayosababisha uharibifu wa misitu.
Mh. Kheri amesema utafiti unaonesha kuwa uchomaji moto wakati wa maandalizi ya mashamba, matumizi ya moto katika uvunaji wa asali kwa njia za jadi, pamoja na vitendo vya chuki binafsi miongoni mwa wananchi, ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuibuka na kusambaa kwa moto katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, taarifa ya mapambano dhidi ya moto iliyotolewa na Uongozi wa Kijiji cha Kidete imeeleza kuwa Mradi wa FORLAND umekuwa ukitoa miche rafiki kwa mazingira, hatua ambayo imechangia wananchi kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Hata hivyo, kupitia Mradi wa FORLAND, Mkoa wa Iringa umeendelea kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya majanga ya moto kupitia kamati za vijiji, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza misitu na mazingira.
Mradi wa FORLAND na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wanaendelea kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda misitu, wakisisitiza kuwa uhifadhi wa misitu ni kulinda uchumi, mazingira na maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.