Nuru FM

Mafinga mji wakanusa madaktari saba kufutwa kazi

29 August 2026, 09:48

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mheshimiwa Reginant Kivinge akizungumza katika baraza la Madiwani. Picha na Fredick Siwale

“Huku Mafinga hakuna watumishi walioadhibiwa kwa utovu wa nidhamu”

Na Fredrick Siwale

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Mafinga Mkoani Iringa limekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa Halmashauri hiyo imewafukuza kazi na kuwaadhibu baadhi ya watumishi kwa sababu za utovu wa nidhamu.

Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mheshimiwa Reginant Kivinge, amesema taarifa hizo si za kweli, akisisitiza kuwa hakuna mtumishi aliyefukuzwa kazi wala kuadhibiwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu kama inavyodaiwa.

Sauti ya Kivinge

Aidha, amewataka wananchi kutofautisha kati ya maoni ya mtu binafsi na taarifa rasmi za Halmashauri, huku akiwataka kuhakikisha wanathibitisha taarifa zinazohusu taasisi hiyo kupitia vyanzo rasmi kabla ya kuzisambaza.

“Kama Mwenyekiti wa Halmashauri, nakanusha taarifa hiyo. Hatujafukuza watumishi, pia hakuna watumishi walioadhibiwa kwa utovu wa nidhamu. Halmashauri iko vizuri na kila mtumishi katika idara yake anaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa. Mafinga ni salama na tunaendelea kuchapa kazi,” amesema Kivinge.

Kivinge amesisitiza kuwa Halmashauri ya Mji Mafinga inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa utulivu, huku watumishi wakiendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi na kuzingatia majukumu yao ya kazi.

Sauti ya Kivinge
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Peter Ngusa

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Peter Ngusa, amesema hakuna daktari yeyote aliyefukuzwa kazi na kwamba madaktari wote waliopo katika Halmashauri hiyo wanaendelea na ajira zao kama kawaida.

Ngusa pia amesema hakuna watumishi walioondolewa kwenye majukumu ya kada zao na kupelekwa kwenye majukumu mengine, kama inavyodaiwa kwenye taarifa hizo zinazosambaa mitandaoni.

Sauti ya Ngussa