Nuru FM

CCM yakagua mradi wa hewa tiba Mafinga Mji

15 July 2026, 10:32

Mwenyekiti wa Kamati ya siasa Mkoa wa Iringa Daudi Yassin na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James katika ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo Mafinga Mji. Picha na Hafidh Aally

Mtambo huo utawezesha upatikanaji wa hewa tiba kwa wakati, kupunguza gharama za ununuzi na usafirishaji wa oksijeni kwa wagonjwa Mafinga Mji.

Na Hafidh Ally

Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuzalisha hewa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga, uliotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Daudi Yassin, amesema kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha sekta ya afya kwa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, hatua itakayochangia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.

Sauti ya Daud Yassin

Yassin ameipongeza Serikali kwa kupeleka mradi huo katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga, akisema umeongeza upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi huku akiwataka watumishi wa hospitali kuutunza na kuusimamia vizuri mtambo huo ili uweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Sauti ya Daud Yassin

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Dkt. Bonaventura Chitopela, amesema hospitali hiyo hupokea wastani wa wagonjwa 650 kwa siku, hali inayosababisha mahitaji makubwa ya hewa tiba.

Ameeleza kuwa uwepo wa mtambo huo utawezesha upatikanaji wa hewa tiba kwa wakati, kupunguza gharama za ununuzi na usafirishaji wa oksijeni, pamoja na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa uhakika kwa wagonjwa wa dharura, watoto wachanga, wajawazito na wagonjwa mahututi.

Sauti ya Mganga Mkuu Mafinga

Mtambo huo una uwezo wa kuzalisha hadi mitungi 60 ya hewa tiba kwa siku, hatua inayotarajiwa kupunguza utegemezi wa ununuzi wa oksijeni kutoka maeneo ya mbali, kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali na kuboresha huduma za dharura pamoja na matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji oksijeni.