Nuru FM
Nuru FM
30 April 2026, 11:28

Mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kuwasaidia wakulima kusimamia mapato yao baada ya mavuno kwa ufanisi.
Na Ayoub Sanga
Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU) kimeendesha mafunzo maalum ya ujasiriamali kwa wanawake wanachama wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) yakilenga kufanya kilimo kama biashara yenye tija na si shughuli ya kujikimu pekee huku yakisisitiza umuhimu wa kujiepusha na mikopo umiza.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Iringa Dk. Deo Sabokwigina ambaye amewajengea uwezo washiriki katika maeneo ya nidhamu ya fedha baada ya mavuno, umuhimu wa kujiunga na vikundi vya kifedha (VICOBA) pamoja na nguvu ya ushirikiano katika kukuza uchumi wa kaya na jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Katika ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Iringa, Manispaa ya Iringa Dk. Sabokwigina ambaye ni Mkufunzi wa mafunzo hayo amesisitiza kuwa kilimo cha kisasa kinahitaji mabadiliko ya fikra akieleza kuwa mkulima anapaswa kuchukulia shughuli hiyo kama biashara inayohitaji mipango madhubuti, nidhamu ya kifedha na maamuzi sahihi.
Kwa upande wake, Afisa Miradi wa IFCU, William Seme amesema mafunzo hayo yamefanyika chini ya mradi unaofadhiliwa na Shirika la We Effect kutoka Sweden akibainisha kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya wakulima kuendelea kuchukulia kilimo kama shughuli ya kawaida.
Kwa upande wao Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamepata manufaa makubwa ikiwemo mbinu za kuweka akiba, kuandaa bajeti na kuwa makini na mikopo wanayochukua ili kuepuka mikopo umiza.
Mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kuwasaidia wakulima kusimamia mapato yao baada ya mavuno kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuweka akiba kwa ajili ya msimu ujao, kutunza kumbukumbu za kifedha, na kufanya uwekezaji wenye tija.