Nuru FM

Waziri Mkuu kufanya ziara Mkoani Iringa

1 May 2026, 09:25

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James akizungumza na wanahabari kuhusu ujio wa Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba. Picha na Ayoub Sanga.

Ziara hiyo ni Sehemu ya serikali kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi moja kwa moja.

Na Ayoub Sanga

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ametangaza kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Iringa kuanzia Mei 2 hadi 3, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari Mhe. Kheri amesema kuwa katika ziara hiyo, Waziri Mkuu atatembelea Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi pamoja na Halmashauri ya Mji wa Mafinga, akihusisha majimbo matatu ambayo ni Mufindi Kaskazini, Mufindi Kusini na Mafinga Mjini.

Mhe. Kheri ameeleza kuwa siku ya kwanza ya ziara hiyo, Mei 2, 2026, Mhe. Dkt. Nchemba atafanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Igowole kilichopo Jimbo la Mufindi Kusini, ambapo atapata fursa ya kuwasikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zao, aidha, atatembelea barabara ya Mtiri – Ifwagi na kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Mufindi Kaskazini.

Sauti ya Kheri

Pia Mhe. Kheri, amesema kuwa siku ya pili ya ziara, Mei 3, 2026, Waziri Mkuu ataendelea na mkutano wa hadhara pamoja na kupokea na kusikiliza kero na taarifa mbalimbali za maendeleo kutoka kwa viongozi wa serikali katika sekta tofauti.

Sauti ya Kheri

Mhe. Kheri amewataka wananchi pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara hiyo ili kuwasilisha kero na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu.

Sauti ya Kheri