Wananchi walalamikia kushuka kwa bei ya mazao
21 July 2026, 10:22

Wananchi wameeleza kuwa gharama za mbolea zimeendelea kupanda na kuwa mzigo mkubwa kwa wakulima huku wakilalamikia kuhuka kwa bei za mazao.
Na Hafidh Ally
Wananchi wa Kata ya Ulanda, Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, wamelalamikia kushuka kwa bei za mazao ya kilimo sambamba na kuongezeka kwa gharama za mbolea, hali wanayosema inaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa wakulima.
Wakizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, wananchi wa vijiji vya Mwambao, Weru, Lupalama na Kibebe walisema kuwa licha ya kutumia gharama kubwa kununua mbolea na kuzalisha mazao, bei ya mazao imeendelea kushuka na kuathiri kipato chao pamoja na ustawi wa familia zinazotegemea kilimo.
Wananchi hao pia wameiomba Serikali kuongeza upatikanaji wa mbolea za ruzuku na kuwatafutia masoko ya uhakika kwa mazao yao ili kuboresha kipato cha wakulima.

Akijibu hoja kuhusu mbolea za ruzuku na masoko ya mazao, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, alisema Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa baadhi ya mbolea muhimu, ikiwemo Urea na DAP. Alifafanua kuwa aina nyingine za mbolea ziliondolewa kwenye mpango wa ruzuku baada ya kipindi cha mpito kilicholenga kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbolea hizo.
Aidha, Kiswaga alisema Tanzania inatumia mfumo wa soko huria, hivyo uzalishaji unapokuwa mkubwa bei za mazao hushuka kutokana na wingi wa bidhaa sokoni ambapo Serikali inaendelea na mipango ya kuweka bei elekezi za ununuzi na uuzaji wa mazao ili kulinda maslahi ya wakulima.
Katika ziara hiyo, Mbunge Kiswaga alikabidhi mabati 70 kwa Kijiji cha Mwambao kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji na nyumba ya watumishi, akiyawakabidhi kwa viongozi wa kijiji hicho.
