Wananchi Ihalimba waomba ukarabati wa barabara
14 September 2026, 10:11

Barabara za Kata ya Ihalimba wamelalamikia ubobu wa barabara hasa katika kipindi cha mvua.
Na Fredrick Siwale
Wananchi wa vijiji vilivyopo Kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, wameiomba Serikali kukarabati barabara za maeneo yao, wakieleza kuwa barabara hizo hazipitiki vizuri, hususan wakati wa msimu wa mvua.
Ombi hilo limetolewa na Diwani wa Kata ya Ihalimba, Mhe. Different Lufyagile, wakati wa ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Mhe. Exaud Kigahe, ambapo ameeleza kuwa ubovu wa barabara umekuwa ukisababisha adha kwa wananchi na kuathiri shughuli zao za kila siku.
Akijibu changamoto hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Mhe. Exaud Kigahe, amesema Serikali imeweka mpango wa kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 44 kwa kiwango cha lami katika jimbo hilo, hatua inayolenga kuboresha miundombinu ya usafiri na kupunguza kero kwa wananchi.

Mhe. Kigahe amesema utekelezaji wa mpango huo utasaidia kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Mufindi Kaskazini.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kigahe pia ameahidi kuongeza juhudi katika kufuatilia upatikanaji wa jokofu la kuhifadhia maiti katika eneo hilo, akieleza kuwa chumba cha kuhifadhia maiti tayari kimejengwa na kinachohitajika ni kukamilisha upatikanaji wa vifaa muhimu ili kiweze kuanza kutumika.