Wanahabari Iringa wapewa elimu ya matumizi ya Maziwa
29 May 2026, 10:36

Maziwa ni chakula muhimu na kamili kwa watu wa rika zote kutokana na kuwa na makundi yote ya virutubishi muhimu kwa mwili wa binadamu.
Na Hafidh Ally
WAANDISHI wa habari mkoani Iringa wamepatiwa elimu kuhusu matumizi ya maziwa bora na salama pamoja na kuhamasishwa kushiriki katika uwekezaji wa uzalishaji, ukusanyaji, usafirishaji na usindikaji wa maziwa ili kuongeza thamani ya zao hilo nchini.
Elimu hiyo imetolewa katika maadhimisho ya Wiki ya Unywaji Maziwa yaliyofanyika mkoani humo, ambapo wadau wa sekta ya mifugo na maziwa walieleza umuhimu wa matumizi ya maziwa yaliyo salama kwa afya ya jamii na kukuza uchumi wa wafugaji.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari mkoani Iringa, Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof George Msalya, amesema waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya maziwa salama pamoja na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa tasnia hiyo.
Profesa Msalya amesema maziwa ni chakula muhimu na kamili kwa watu wa rika zote kutokana na kuwa na makundi yote ya virutubishi muhimu kwa mwili wa binadamu.
“Maziwa ni dhahabu nyeupe. Ni chakula cha asili na bora kwa wakati wote na kwa watu wote. Mtu anahitaji angalau glasi moja ya maziwa kwa siku na wastani wa lita 200 kwa mwaka,” amesema Profesa Msalya.
Amesema matumizi ya maziwa yasiyo salama yanaweza kusababisha madhara ya kiafya, hivyo jamii inapaswa kuhakikisha maziwa wanayotumia yanatoka katika vyanzo vinavyoaminika na vinavyofuata taratibu za usafi na ubora.
Katika kuleta mageuzi hayo, Mradi wa TI3P unaosimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Heifer International na Land O’Lakes Venture37, unalenga kuwaunganisha wafugaji na wasindikaji wa maziwa ili kuongeza tija katika uzalishaji na biashara ya maziwa.
Mwakilishi wa Benki ya Kilimo, Joseph Mabula, amesema mradi huo umewezeshwa kwa zaidi ya dola milioni 37 kwa ajili ya mikopo na uwekezaji katika sekta ya maziwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha huduma za mikopo zinawafikia wafugaji na wasindikaji wa maziwa ili kuongeza uzalishaji na tija. Tunatekeleza mradi huu katika mikoa 15 nchini,” amesema Mabula.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Mnyororo wa Thamani wa Tasnia ya Maziwa, Mbehoma Peternus, amesema Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) ni mradi wa miaka 10 wenye thamani ya dola milioni 231 unaolenga kuboresha uzalishaji wa maziwa kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.
Amesema mradi huo utaleta ng’ombe 8,600 wenye mimba kutoka nje ya nchi ambapo 600 watapelekwa Zanzibar huku wengine wakisambazwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuanzisha kizazi kipya cha wafugaji wenye tija.
“Mwisho wa mradi tunatarajia kuwa na zaidi ya ng’ombe 24,500 wa kisasa watakaozalishwa hapa nchini na kuongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa maziwa,” amesema Peternus.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi wa habari wameeleza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuandika habari zenye kuhamasisha jamii kutumia maziwa salama na kuwajengea wafugaji uelewa kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta hiyo.