RC kheri asisitiza nidhamu usimamizi wa mapato
30 June 2026, 09:55

Utaratibu wa Kupeleka fedha Benki utasaidia kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa mapato.
Na Hafidh Ally
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuhakikisha mapato yote yanayokusanywa kupitia vyanzo mbalimbali yanapelekwa benki mara moja ili kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kudhibiti upotevu wa fedha za umma.
Akizungumza katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo uliojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2026, Mhe. Kheri amesema kuwa nidhamu katika usimamizi wa mapato ni msingi wa maendeleo ya halmashauri.
Mhe. Kheri amesema kuwa watendaji wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato wanapaswa kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinawasilishwa benki kwa wakati kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali, ili kuondoa mianya ya upotevu wa fedha.
Aidha, Mhe. Kheri amesisitiza kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuyasimamia kwa ufanisi ili yaweze kuchangia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Mhe. Kheri amewataka viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo kufanya tafiti na ubunifu wa kiuchumi ili kubaini fursa nyingine za mapato, huku akisisitiza uwazi, uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Siwema Jumaa amesema kuwa Wilaya ya Kilolo imeendelea kupokea maombi kutoka kwa wawezekazaji ambao wameonesha nia ya kutaka maeneo ili kuwekeza wilayani humo.
Hata hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imepongeza na Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kupata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, akisema kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa usimamizi mzuri wa fedha za umma na uwajibikaji wa viongozi pamoja na watendaji wa halmashauri hiyo.
