Nuru FM

Kiswaga achangia Mbao Jengo la Mama na Mtoto Lumuli

9 July 2026, 08:55

Mbunge wa Jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga akikabidhi Mbao. Picha na Hafidh Ally

Katika kusukuma mbele utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili, Mbunge Kiswaga ameendelea kutimiza ahadi zake katika jimbo la Kalenga.

Na Hafidh Ally

Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, amechangia mbao zenye thamani ya shilingi milioni 1.17 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika Kata ya Lumuli, wilayani Iringa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata hiyo, Kiswaga alisema mchango huo unaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Katika ziara hiyo, Mbunge huyo amekutana na wananchi wa vijiji vya Isupilo, Itengulinyi, Lumuli na Muwimbi, ambapo aliwashukuru kwa kuendelea kumuamini na kumpa ridhaa ya kuwatumikia kwa muhula wa pili kama Mbunge wa Jimbo la Kalenga.

Sauti ya Kiswaga

Aidha, Kiswaga amesema Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Lumuli, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wa eneo hilo.

Amesisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na Serikali na wananchi katika kusukuma mbele miradi ya maendeleo ili kuboresha sekta za afya, elimu na huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi wa Jimbo la Kalenga.