Nuru FM

Mifugo 345 imekamatwa ndani ya Hifadhi ya Ruaha.

15 November 2023, 11:50 am

Mifugo iliyokamatwa na Askari wa Hifadhi ya Ruaha.

Na Mwandishi Wetu.

Jumla ya Mifugo 345 Imekamatwa ikichungwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha kinyume cha sheria za uhifadhi.

Hayo yamezungumzwa na
Godwell Ole Meing’ataki
Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Kamanda wa Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuongeza kuwa huo ni mwendelezo wa Hifadhi ya Ruaha katika kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa mazingira ndani ya hifadhi na hususan katika bonde la oevu la Usangu ambapo kuna vyanzo muhimu vya maji kwa ajili ya mto Ruaha Mkuu na bioanuai muhimu kwa mazingira, uhifadhi na utalii.

Meing’ataki amesema kuwa Mifugo hiyo Imekamatwa baada ya Askari wa Doria kubaini kuwepo kwa baadhi ya wafugaji ambao wanaendelea kukiuka kwa makusudi maelekezo ya Serikali na sheria za hifadhi kwa kuingiza mifugo hifadhini, na kubuni mbinu ya kuingiza mifugo hifadhini wakati wa usiku na kuiondoa mapema sana asubuhi.

Mhifadhi huyo amebainisha kuwa vikosi vya askari wa doria pia wamefanikiwa kukamata wavamizi wanaolima
ndani ya hifadhi katika maeneo ambayo hayaruhusiwi ambapo katika doria hiyo Tractor moja aina ya Solanika inashikiliwa wakati taratibu za kufilishwa vyombo vya sheria zinaendelea.

Katika hatua nyingine Meing’ataki Ametoa wito kwa wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kutii sheria , kanuni na kuzingatia maelekezo ya Serikali juu ya kuheshimu na kuzingatia sheria za hifadhi na kutoingia hifadhini au kuingiza mifugo hifadhini na kitojihusisha na shughuli ya uvuvi haramu kwani atakayebainika atachukuliwa sheria.

Aidha, vikosi vya doria katika hifadhi na ofisi ya Naibu Kamishna Kanda ya Kusini wapo kazini muda wote tayari kukabiliana na wahalifu wote wanaokiuka sheria na kanuni za hifadhi.

Amesema Hifadhi inaendelea kushirikiana viongozi, ofisi ya Kanda ya Kusini TANAPA, wadau na wananchi katika kutoa elimu ya uhifadhi juu ya umuhimu wa kuendelea kulinda na kutunza hifadhi ya Ruaha kwa maslahi mapana kwa Taifa na kama
urithi wa kizazi kijacho.